📌 Kamera Kufungwa Kudhibiti Uharibifu

Wizara ya Ujenzi kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Kigoma imetoa rai kwa wananchi wanaoishi pembezoni mwa miundombinu ya barabara kushiriki kikamilifu katika kulinda na kutunza miundombinu hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kuendelea kuwa salama kwa watumiaji.

Rai hiyo imetolewa na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kigoma, Mhandisi Elsony Mweladzi, ambaye amesema kuwa mkoa huo una jumla ya madaraja 396, yakiwemo madaraja makubwa matano ambayo yote yako katika hali nzuri na salama kwa matumizi ya wananchi.

Mhandisi Mweladzi amesema ni muhimu wananchi kutunza na kulinda uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika miundombinu ya barabara na madaraja ili kuepusha hasara zinazoweza kujitokeza kutokana na vitendo vya uharibifu.

“Niwasihi wananchi wanaoishi maeneo yanayopitiwa na barabara, hususan eneo la Malagarasi katika Daraja la Kikwete, kutunza miundombinu iliyowekwa ikiwemo taa za barabarani kwa kuepuka kuzihujumu na hivyo kuisababishia Serikali gharama za kufunga taa mpya,” amesema Mhandisi Mweladzi.

Aidha, amesema TANROADS ina mpango wa kuimarisha usalama wa madaraja kwa kufunga kamera za ulinzi zitakazosaidia kulinda mali zilizowekwa katika miundombinu hiyo.

Katika hatua nyingine, Mhandisi Mweladzi ametoa rai kwa madereva kuzingatia matumizi sahihi ya barabara kwa kuepuka kufanya matengenezo ya magari barabarani, kumwaga mafuta na kuhakikisha magari makubwa yanayobeba bidhaa, mchanga au mizigo mingine yanafunikwa vizuri ili kuzuia kumwagika kwa mizigo hiyo barabarani.

Pia, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kutoa fedha za kuimarisha miundombinu ya barabara na madaraja katika Mkoa wa Kigoma.

Amesema uwekezaji huo umechangia kwa kiasi kikubwa kuufungua Mkoa wa Kigoma kiuchumi na kijamii kupitia ujenzi wa barabara za kiwango cha juu pamoja na uwekaji wa taa za barabarani.