WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali itaendelea kupambana na biashara ya bidhaa bandia kwa kuwa zinakwamisha ukuaji wa viwanda, sekta binafsi pamoja na kuhatarisha maisha ya wananchi.

Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali itachukua hatua kali kwa wawekezaji wanaofanya utapeli na uhujumu uchumi kwa kuanzisha kampuni kwa kutumia majina ya Watanzania huku kampuni hizo zikiwa ni za kwao jambo ambalo halikubaliki.

Ametoa kauli hiyo leo (Jumatano, Juni 24, 2026) alipomwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye ufunguzi wa Kituo cha Huduma za Magari cha Superdoll na Chuo cha Mafunzo ya Usafiri na Usalama Barabarani kilichopo jijini Dodoma.

Mheshimiwa Dkt. Mwigulu amesema bidhaa bandia zinakwamisha jitihada za ujenzi wa viwanda na kukuza sekta binafsi na pia zimekuwa chanzo cha ajali, hasara za kiuchumi na wakati mwingine zinasababisha vifo na ulemavu wa kudumu kwa wananchi, hivyo hakuna nafasi ya kuendelea kuvumilia vitendo hivyo.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kufuatilia na kuwachukulia hatua kali wawekezaji wanaofanya vitendo vya udanganyifu, uvunjifu wa sheria na hujuma dhidi ya uchumi wa Taifa kwa kufungua makampuni kwa kutumia majina ya wazawa.

Waziri Mkuu ameyasema hayo baada ya Serikali kubaini kuwepo kwa baadhi ya wawekezaji wanaotumia majina na taarifa za Watanzania kuanzisha kampuni za kizawa kwa lengo la kupata fursa zinazotengwa kwa wazawa, ilhali umiliki na manufaa yote ya kampuni hizo hubaki mikononi mwao.

Awali, Waziri Mkuu alizitaka taasisi zote za Serikali kuhakikisha zinatumia vipuri halisi ili kupunguza gharama za matengenezo, kuongeza usalama wa vyombo vya moto na kuepuka matumizi ya bidhaa bandia katika shughuli za Serikali.

Akizungumzia ushiriki wa Watanzania katika uchumi wa nchi yao, Waziri Mkuu amesema Tanzania inaendelea kuthamini mchango wa wawekezaji na sekta binafsi, lakini haitakubali vitendo vya ubinafsi vinavyowanyima Watanzania fursa walizostahili kwa mujibu wa sheria.

Pia, Waziri Mkuu ameipongeza kampuni ya Superdoll kwa uwekezaji huo mkubwa akisema ni ushahidi kuwa Watanzania wana uwezo wa kujenga, kuendesha na kukuza kampuni zinazoweza kushindana katika viwango vya kimataifa huku zikichangia ajira, mafunzo ya ujuzi na maendeleo ya uchumi wa Taifa.

Amesema kituo hicho tayari kimechangia kutoa mafunzo kwa zaidi ya vijana 100 na kutoa ajira kwa mamia ya Watanzania wakati wa utekelezaji wa mradi huo. “Serikali imejivunia kuona kampuni za Kitanzania zilizojengwa na Watanzania, zinaendeshwa na Watanzania na zinaendelea kuwekeza kwa ajili ya Watanzania wote.”

Kwa upande wake, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema uwekezaji huo utachangia kuimarisha usalama barabarani, kuongeza ujuzi wa madereva na wataalamu wa usafiri, kuendeleza matumizi ya teknolojia za kisasa na kuandaa rasilimali watu wenye uwezo wa kushindana katika soko la ajira la kikanda na kimataifa.

Profesa Mbarawa pia alieleza umuhimu wa kuendelea kuboresha mazingira ya matumizi ya teknolojia mpya katika sekta ya usafirishaji, ikiwemo matumizi ya matairi ya “super single”, ili kuongeza ushindani wa wasafirishaji wa Tanzania katika masoko ya kikanda.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Superdoll, Seif Ali Seif amesema kituo hicho ni sehemu ya utekelezaji wa maono ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuendelea kuimarisha uwekezaji, huduma za kisasa, mafunzo na usalama katika sekta ya usafirishaji nchini.

Amesema kampuni hiyo itaendelea kuwekeza katika maendeleo ya rasilimali watu, teknolojia na huduma bora kwa lengo la kuchangia ukuaji wa uchumi wa Taifa na kuongeza fursa za ajira kwa vijana wa Kitanzania.

Hafla hiyo imehudhuriwa na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega; Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga; Waziri wa Madini, Anthony Mavunde na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir.

Wengine ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule; Balozi wa Morocco, Balozi wa Oman, mwakilishi wa Balozi wa Ufaransa; viongozi wa taasisi za kifedha; viongozi wa dini; washirika wa maendeleo pamoja na viongozi wengine wa Serikali na sekta binafsi.