NA DENIS MLOWE IRINGA 

ZAIDI ya vijana 200 kutoka vijiji 61 vinavyozunguka Shamba la Miti la Taifa la Sao Hill wilayani Mufindi, mkoani Iringa, wamehitimu mafunzo maalumu ya kukabiliana na majanga ya moto wa misitu ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ulinzi wa rasilimali za misitu na mazingira kwa ujumla.

Mafunzo hayo yametolewa baada ya kufanyika mchakato wa usaili uliowahusisha zaidi ya vijana 400 waliojitokeza kupima utimamu wa mwili na akili kwa lengo la kushiriki katika kikosi cha kukabiliana na moto wa misitu hatua hiyo imeelezwa kuwa ni mkakati wa kuhakikisha kunakuwa na nguvu kazi ya kutosha yenye uelewa wa masuala ya usalama wa misitu katika maeneo yanayozunguka shamba hilo kubwa la miti.

 

Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Msaidizi wa Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti la Taifa la Sao Hill, PCO Said Singano, alisema ushirikishwaji wa vijana kutoka vijiji vinavyozunguka shamba hilo ni njia bora ya kujenga uelewa wa pamoja kuhusu umuhimu wa kulinda misitu na kuzuia hasara zinazoweza kusababishwa na moto.

 

 

Alisema moto wa misitu umekuwa tishio kubwa katika maeneo mbalimbali ya misitu nchini, hivyo ni muhimu kuendelea kutoa elimu na mafunzo kwa wananchi wanaoishi karibu na maeneo hayo ili wawe sehemu ya suluhisho la changamoto hiyo. 

Aliongeza kuwa vijana waliopatiwa mafunzo wamefundishwa mbinu mbalimbali za kutambua vihatarishi vya moto, namna ya kuzuia kuenea kwa moto pamoja na hatua za haraka za kuchukua pindi moto unapozuka.

 

Singano alisema kuwa ushiriki wa wananchi katika shughuli za uhifadhi umeendelea kuleta matokeo chanya kwa kuwa jamii imekuwa na uelewa mkubwa zaidi kuhusu thamani ya misitu katika maendeleo ya kiuchumi na uhifadhi wa mazingira. 

 

Alibainisha kuwa Shamba la Miti la Taifa la Sao Hill linaendelea kushirikiana na vijiji vinavyolizunguka ili kuhakikisha misitu inalindwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

 

 

Kwa upande wake, Afisa wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Mufindi, Sajenti Guntramu Mlenge, alisema ushirikiano uliopo kati ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji pamoja na Shamba la Miti la Sao Hill umechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu namna ya kujikinga na majanga ya moto.

 

Alisema kupitia mafunzo hayo, vijana wamepata maarifa ya kutumia vifaa vya kuzimia moto, kutengeneza njia za kuzuia moto kuenea pamoja na mbinu za kufanya doria katika maeneo yenye hatari kubwa ya kutokea kwa moto. A

 

Aidha, alieleza kuwa elimu hiyo itawasaidia vijana kuwa mabalozi wa usalama wa mazingira katika vijiji vyao.

 

Baadhi ya vijana walioshiriki mafunzo hayo wameeleza kufurahishwa na fursa waliyoipata wakisema kuwa imewaongezea ujuzi na kuwapa nafasi ya kushiriki moja kwa moja katika shughuli za kulinda misitu. 

 

Walisema maarifa waliyojifunza yatawasaidia kutoa elimu kwa wananchi wengine kuhusu madhara ya moto wa misitu na umuhimu wa kuhifadhi mazingira.

 

Hatua ya kuwajengea uwezo vijana katika maeneo yanayozunguka Shamba la Miti la Taifa la Sao Hill inaonekana kuwa sehemu muhimu ya mkakati wa kupunguza matukio ya moto wa misitu ambayo yamekuwa yakisababisha hasara kubwa kwa mazingira, uchumi na maendeleo ya jamii. 

Serikali na wadau wa uhifadhi wanaamini kuwa ushiriki wa wananchi, hususan vijana, ni nguzo muhimu katika kuhakikisha misitu inalindwa na kuendelea kuwa rasilimali yenye manufaa kwa taifa.