Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma 

Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vipimo (WMA),Fransis Olwero , amesema kuwa maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026 yametoa fursa muhimu kwa taasisi hiyo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa matumizi sahihi ya vipimo katika shughuli mbalimbali za kila siku.

Akizungumza na waandishi wa habari Juni 23,2026 katika banda la WMA kwenye maadhimisho ya wiki ya utumishi wa umma 2026 jijini Dodoma, amebainisha Kuwa wananchi walipata elimu kuhusu faida za vipimo katika maisha ya kila siku na shughuli za kiuchumi.

Huku akibainisha kuwa karibu asilimia kubwa ya shughuli za maisha ya kila siku nchini zinahusisha vipimo, hivyo ni muhimu wananchi kuelewa na kuzingatia matumizi sahihi ya vipimo ili kuongeza ufanisi na uwazi katika biashara.

Ameongeza kuwa WMA imekuwa ikitoa elimu kwa wananchi, wawekezaji pamoja na watumishi wa umma waliotembelea banda hilo, ambapo wengi wao wameonesha kufaidika na elimu hiyo ya vipimo.

Amesema kuwa katika sekta ya kilimo, wakulima na wafanyabiashara wanapaswa kununua na kuuza mazao kwa kutumia vipimo sahihi badala ya kutumia makadirio au magunia yasiyo na viwango vinavyotambulika.

Amebainisha kuwa mfumo wa kununua na kuuza kwa vipimo utasaidia kuondoa changamoto ya udanganyifu katika biashara ya mazao, hususan wakati wa msimu wa mavuno.

Ameongeza kuwa WMA inaendelea kutoa wito kwa wakulima, wanunuzi na madalali kuzingatia matumizi ya vipimo ili kuhakikisha biashara inakuwa ya haki na yenye uwazi.

Pia amebainisha kuwa sheria za vipimo zipo na zinaelekeza matumizi sahihi ya vipimo, na kwamba yeyote atakayekiuka taratibu hizo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.