Na John Bukuku, Dar es Salaam
Katika bara la Afrika, Botswana imeendelea kutajwa kama mfano wa nchi iliyofanikiwa kutumia rasilimali zake za madini, hususan almasi na dhahabu, kama kichocheo cha maendeleo ya taifa. Mafanikio hayo hayakutokana na wingi wa rasilimali pekee, bali yalijengwa kupitia mfumo makini wa usimamizi unaoweka mbele sheria, utaalamu na uwezo wa wataalamu wa ndani katika kulinda maslahi ya nchi.
Botswana ilitambua mapema kuwa rasilimali za taifa zinaweza kuwa neema au changamoto kutegemeana na uwezo wa serikali kusimamia mikataba yake na makampuni ya kimataifa. Kwa msingi huo, serikali yake iliwekeza kwa kiasi kikubwa katika kuwaandaa wataalamu wake wakiwemo wanasheria, wachumi, wataalamu wa kodi na biashara za kimataifa ili wawe na uwezo wa kujadiliana kwa usawa na wawekezaji wakubwa duniani.
Rais wa Jamhuri ya Botswana Mhe. Duma Boko.
Mfumo huo uliiwezesha Botswana kuingia katika makubaliano yenye manufaa zaidi kwa taifa, ikiwemo ushirikiano wake na kampuni ya De Beers kupitia kampuni ya pamoja ya Debswana katika sekta ya almasi. Serikali haikubaki katika nafasi ya kukusanya kodi pekee, bali ilihakikisha inakuwa sehemu ya umiliki na maamuzi ya kimkakati ili wananchi wanufaike zaidi kupitia mapato na gawio la uwekezaji.
Jambo kubwa lililojenga mafanikio ya Botswana ni kuwa na wataalamu wenye uwezo wa kuchambua mikataba kwa kina kabla ya kusainiwa. Taifa hilo liliweka mkazo katika kujenga uwezo wa ndani badala ya kutegemea wataalamu wa nje pekee, jambo lililosaidia kulinda rasilimali zake na kuhakikisha mikataba inazingatia maslahi ya muda mrefu ya wananchi.
Uzoefu huo unatoa somo muhimu kwa Tanzania ambayo nayo ina utajiri mkubwa wa madini, gesi na maliasili mbalimbali. Katika miaka ya nyuma kulikuwa na mijadala kuhusu namna taifa lilivyokuwa linanufaika na rasilimali zake, hali iliyosababisha Serikali kufanya mageuzi mbalimbali ya kisheria na kitaasisi ili kuongeza ulinzi wa maslahi ya taifa.
Mwaka 2017 ulikuwa hatua muhimu katika historia ya usimamizi wa rasilimali Tanzania baada ya Serikali kufanya marekebisho ya sheria mbalimbali zinazohusu sekta ya madini na rasilimali za taifa. Mageuzi hayo yalilenga kuimarisha mamlaka ya Serikali katika kusimamia mikataba, kuongeza uwajibikaji na kuhakikisha rasilimali zinakuwa na mchango mkubwa kwa maendeleo ya wananchi.
Katika utekelezaji wa mwelekeo huo, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imekuwa mstari wa mbele katika kujenga uwezo wa wataalamu wake ili kuhakikisha mikataba mikubwa ya uwekezaji inapitiwa kwa umakini wa kitaalamu kabla ya Serikali kufanya maamuzi.
Mhe. Johari Hamza Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Kwa Mujibu wa Ofisi ya Mawanasheria Mkuu wa Serikali inasema katika kipindi hicho, Serikali imewekeza katika kuwajengea uwezo mawakili wake kupitia mafunzo mbalimbali ndani na nje ya nchi. Jumla ya mawakili wa Serikali 115 walipatiwa mafunzo ndani ya nchi katika maeneo mbalimbali muhimu ya kisheria yanayohusiana na uchumi na rasilimali za taifa, yakiwemo sheria za sekta ya mafuta na gesi, madini, mazingira, nishati, bima, hifadhi ya jamii, usafirishaji wa majini pamoja na masuala ya ubia kati ya Serikali na sekta binafsi (PPP).
Aidha, mawakili wa Serikali 69 walipatiwa mafunzo nje ya nchi katika maeneo ya kimkakati kama majadiliano na usuluhishi wa mikataba ya uwekezaji katika sekta ya mafuta na gesi, uandishi wa mikataba, usuluhishi wa migogoro ya kimataifa, manunuzi na miradi ya taasisi za fedha za kimataifa pamoja na sheria za biashara na uwekezaji wa kimataifa katika nchi mbalimbali ikiwemo Afrika Kusini, Eswatini, Kenya, Falme za Kiarabu, Canada na Japan.
Mbali na mafunzo hayo, jumla ya watumishi 16 wanaendelea na masomo ya muda mrefu katika maeneo mbalimbali ya kitaalamu ikiwemo Shahada za Uzamili katika Sheria za Biashara za Kimataifa na Uwekezaji, Njia Mbadala za Utatuzi wa Migogoro (ADR), Sheria za Kampuni, Sheria za Kazi, Usalama wa Mifumo ya Tehama, Usimamizi wa Rasilimaliwatu pamoja na maeneo mengine yanayolenga kuongeza uwezo wa taasisi.
Hatua hizi zinaonyesha mabadiliko ya kimkakati ambapo Tanzania inalenga kuwa na kizazi cha wataalamu wenye uwezo wa kusimamia majadiliano ya mikataba mikubwa ya kimataifa kwa kutumia ujuzi wa ndani. Lengo ni kuhakikisha taifa linakuwa na wataalamu wanaoweza kukaa mezani na kampuni kubwa za kimataifa wakiwa na uwezo wa kulinda maslahi ya nchi.
Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili wa Serikali (PBA), Wakili Addo Novemba Mwasongwe.
Mwenyekiti wa Chama cha Mawakili wa Serikali (PBA), Wakili Addo Novemba Mwasongwe. , anasema kuwa mafunzo hayo yamekuwa na mchango mkubwa katika kuongeza uwezo wa kitaaluma kwa mawakili wa Serikali na kuwawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi. Anasema uwekezaji unaofanywa na Serikali katika kuwajengea uwezo watumishi wake umeendelea kuimarisha taaluma ya sheria nchini.
Ameongeza kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imekuwa sehemu muhimu ya kuwaandaa wataalamu hao kabla ya Serikali kuingia katika majadiliano na kusaini mikataba mbalimbali, huku uzoefu wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza Johari katika masuala ya mikataba na makubaliano ukiwa chachu ya kuongeza uelewa kwa mawakili wa Serikali.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan,
Hatua hizi zinaendana na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuhusu utekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2050 ambapo amesisitiza mabadiliko ya mtazamo wa utekelezaji kwa kuondokana na mfumo wa kufanya kazi kwa mazoea na kuanza kutumia mfumo unaozingatia matokeo yanayopimika.
Rais ameagiza kila sekta na taasisi kupitia upya sera na mipango yake ili iendane na Dira ya 2050, sambamba na kufanya marekebisho ya sheria pale inapohitajika ili kujenga mazingira bora ya utekelezaji wa malengo ya taifa. Pia amesisitiza ushiriki mkubwa wa sekta binafsi katika uwekezaji, ubunifu na uanzishaji wa ajira.
Kwa ujumla, safari ya Tanzania ya kujenga uwezo wa wanasheria na wataalamu wake inaonyesha mwelekeo mpya wa kulinda rasilimali za taifa kwa kutumia maarifa, sheria na utaalamu. Kama ilivyo kwa Botswana, nguvu ya Tanzania haitakuwa katika kuwa na rasilimali pekee, bali katika kuwa na watu wenye uwezo wa kuzisimamia kwa manufaa ya wananchi wa sasa na vizazi vijavyo.
