Na John Bukuku
Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imefungua rasmi dirisha la uombaji wa mikopo kwa wanafunzi wanaotarajia kujiunga na vyuo vya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2026/2027, huku ikiweka wazi kuwa maombi hayo yataendelea kupokelewa hadi Agosti 31, 2026.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 19, 2026 katika ofisi za HESLB Kanda ya Mashariki jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo, Dkt. Bill Kiwia, amesema kufunguliwa kwa dirisha hilo ni hatua muhimu inayowawezesha wanafunzi kupata fursa ya kuomba mikopo kwa ajili ya masomo yao ya elimu ya juu.
Amesema dirisha hilo linafunguliwa sambamba na kutangazwa kwa miongozo minne ya utoaji mikopo na ruzuku kwa mwaka wa masomo 2026/2027 ambayo inaeleza sifa, vigezo na taratibu za waombaji.
Ametaja miongozo hiyo kuwa ni Mwongozo wa Utoaji Mikopo kwa Wanafunzi wa Shahada za Awali (Bachelor Degree), Mwongozo wa Utoaji Mikopo kwa Wanafunzi wa Stashahada (Diploma), Mwongozo wa Utoaji Mikopo kwa Stashahada ya Juu ya Mafunzo ya Sheria kwa Vitendo (Postgraduate Diploma in Legal Practice) pamoja na Mwongozo wa Utoaji Ruzuku za Samia (Samia Scholarship).
Dkt. Kiwia amesema miongozo hiyo itapatikana kupitia tovuti ya HESLB ili wanafunzi, wazazi na walezi waweze kuisoma na kuelewa masharti kabla ya kuanza kujaza maombi kupitia mfumo wa mtandao wa Online Loan Application Management System (OLAMS).
Amesisitiza kuwa waombaji wanapaswa kufuata hatua zote muhimu ikiwemo kutembelea tovuti ya HESLB na kuchagua sehemu ya maombi ya mkopo, kujisajili kwa kutumia namba ya mtihani wa Kidato cha Nne na kuhakikisha namba hiyo inafanana na ile watakayotumia wakati wa kuomba udahili chuoni.
Aidha, amesema waombaji wanapaswa kuhakikisha taarifa za vyeti vya kuzaliwa au vifo vya wazazi zimethibitishwa na kupata namba za uhakiki kutoka Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) au Wakala wa Usajili wa Matukio ya Kijamii Zanzibar (ZCSRA).
Kwa waombaji wenye umri wa miaka 18 na kuendelea, Dkt. Kiwia amewataka kujaza Namba ya Utambulisho wa Taifa (NIN), huku akibainisha kuwa wale ambao hawajatimiza umri huo na hawana NIN wataendelea na mchakato wa maombi bila namba hiyo.
Ameongeza kuwa kama ilivyokuwa mwaka wa masomo uliopita, HESLB itaendelea kutumia mfumo wa utambuzi wa waombaji, wazazi na wadhamini kupitia anwani za makazi (NaPA), ambapo mwombaji atatakiwa kuwasilisha kumbukumbu namba iliyopo kwenye barua ya utambulisho kupitia mfumo wa OLAMS.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi huyo amesema kila mwombaji anatakiwa kuwa na akaunti ya benki yenye majina yanayofanana na yale yaliyopo kwenye cheti chake cha Kidato cha Nne (CSEE) ili kurahisisha upatikanaji wa fedha za mkopo.
Kuhusu ruzuku ya Samia Scholarship, Dkt. Kiwia amesema Serikali itaendelea kutoa ufadhili huo kwa wanafunzi wanaofanya vizuri katika masomo ya sayansi kwenye mitihani ya Kidato cha Sita inayoendeshwa na Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA).
Amesema kwa mwaka wa masomo 2026/2027, wanafunzi 1,000 watakaofanya vizuri katika mitihani ya Kidato cha Sita ya mwaka 2026 watanufaika na ufadhili huo, huku orodha ya wanufaika ikitangazwa baada ya matokeo kutolewa.
Aidha, amewahakikishia waombaji kuwa Kituo cha Huduma kwa Wateja cha HESLB kitakuwa wazi katika kipindi cha maombi ili kutoa msaada na ufafanuzi kwa wanafunzi watakaokuwa na changamoto.
Amesema huduma hizo zitapatikana kupitia simu namba 0736 66 55 33, ujumbe wa mfumo jumuishi wa wateja (DOCEP) kupitia 0736 66 55 34, WhatsApp 0739 66 55 33 pamoja na barua pepe [email protected].
Dkt. Kiwia amewataka wanafunzi kutumia muda waliopatiwa vizuri, kusoma miongozo na kujaza taarifa sahihi ili kuhakikisha wanakamilisha maombi yao kabla ya muda wa mwisho wa Agosti 31, 2026.
Amesema HESLB imeendelea kuboresha mfumo wa maombi ya mikopo na sasa umeboreshwa zaidi ili kuwa rafiki kwa watumiaji na kuongeza kasi ya utoaji huduma kwa wanafunzi.

