Na John Bukuku, Dar es Salaam,

Wakili Emma Gelani kutoka Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma amesema Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma inaweka utaratibu mahsusi kuhusu viongozi wanaopaswa kuorodheshwa pamoja na namna ya kushughulikia zawadi wanazopokea ili kulinda uadilifu katika utumishi wa umma.

Akizungumza wakati akiwasilisha mada kuhusu Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma katika kikao kazi kati ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kilichofanyika ukumbi wa PSSSF Juni 19, 2026 jijini Dar es Salaam, Wakili Gelani alisema Kifungu cha 4(1) cha Sheria hiyo kinabainisha orodha ya viongozi wa umma, huku Kifungu cha 30(1) kikimpa mamlaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufanya mabadiliko katika orodha hiyo kwa kuongeza au kupunguza.

Alisema Notisi ya Mabadiliko ya Orodha ya Viongozi wa Umma ya mwaka 2023 ilitangazwa kupitia Tangazo la Serikali (TS) Na. 856 na 857 la tarehe 24 Novemba 2023, likiwa katika lugha ya Kiswahili na Kiingereza.

“Yanapofanyika marekebisho ya wadhifa uliotajwa kama ni Kiongozi wa Umma, wadhifa mpya utahesabika kuwa ndiyo wadhifa sahihi kwa mujibu wa Kifungu cha 30(2),” alisema Wakili Gelani.

Akizungumzia suala la zawadi kwa viongozi wa umma, Wakili Gelani alisema zawadi ni kitu anachopewa mtu bila malipo yoyote kama ishara ya upendo, wema, shukrani, heshima, pongezi au kumbukumbu ya tukio fulani, lakini haipaswi kuwa na dhamira ya kuathiri uamuzi au utekelezaji wa majukumu ya kiongozi.

Alisema Kifungu cha 12(1) cha Sheria hiyo kinakataza viongozi wa umma kujipatia manufaa ya kifedha, huku Kifungu cha 12(1)(e) kikizuia viongozi kuomba au kupokea zawadi zenye manufaa makubwa ya kiuchumi (pecuniary advantage), isipokuwa katika mazingira yanayokubalika kama ukarimu wa kawaida, zawadi kutoka kwa ndugu wa karibu au ukarimu wa kitamaduni.

Wakili Gelani alisema kiongozi anayepokea zawadi yenye thamani inayozidi shilingi 200,000 anatakiwa kutoa tamko la zawadi hiyo na thamani yake kwa Afisa Masuuli ndani ya siku saba kwa mujibu wa Kifungu cha 12(2) pamoja na Kanuni za Maadili ya Viongozi wa Umma.

Alieleza kuwa baada ya kupokea tamko hilo, Afisa Masuuli anatakiwa kuwasilishwa taarifa hiyo pamoja na uamuzi wa matumizi ya zawadi hiyo kwa Kamishna wa Maadili.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa kiongozi haruhusiwi kupokea zawadi yoyote hata kama thamani yake ni pungufu ya shilingi 200,000 endapo zawadi hiyo inaweza kuathiri au kuonekana kuathiri uadilifu wake, utekelezaji wa majukumu yake au kusababisha mazingira ya mgongano wa maslahi.

“Zawadi zinazokatazwa ni pamoja na pesa, burudani, kitu au huduma yoyote inayoweza kuathiri uaminifu wa kiongozi,” alisema.

Alisema dhamira ya sheria hiyo ni kuhakikisha kiongozi wa umma hapokei kitu ambacho kinaweza kumfanya ampendelee mtu au taasisi fulani au kumfanya atoe maamuzi yasiyo ya haki kutokana na zawadi aliyopokea wakati akitekeleza majukumu yake.

Wakili Gelani aliwataka viongozi kujiuliza maswali muhimu kabla ya kupokea zawadi, ikiwemo dhamira ya mtoa zawadi, iwapo wanaweza kuitangaza hadharani bila hofu, pamoja na thamani ya zawadi hiyo.

“Ukiwa na shaka yoyote kuhusu zawadi, usiipokee. Ikiwa unalazimika kuipokea, toa tamko na ipeleke kwa Afisa Masuuli ili aamue matumizi yake,” alisema.

Alisema Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma pamoja na kanuni zake ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha viongozi wanatekeleza majukumu yao kwa uadilifu na kulinda maslahi ya Taifa.