Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Bw. Christopher Ngubiagai akizungumza na wananchi wa kisiwa cha Gana Ukerewe. 
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe Ndg. Vicent Mbua akizungumza na wananchi wa Gana kuachana na uvuvi haramu
…………..
Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Bw. Christopher Ngubiagai, amewataka wananchi wa Kisiwa cha Gana kuendelea kulinda rasilimali za Ziwa Victoria kwa kuepuka matumizi ya nyavu haramu na mbinu nyingine zinazoharibu mazalia ya samaki ili kuhakikisha shughuli za uvuvi zinaendelea kuwa chanzo endelevu cha uchumi kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Bw. Ngubiagai alitoa wito huo Juni 18, 2026, alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kisiwa cha Gana, ambapo alisema kuwa uvuvi ni uti wa mgongo wa uchumi wa visiwa vya Ukerewe na unachangia kwa kiasi kikubwa ajira, biashara na mapato ya Serikali kupitia mazao ya samaki yanayovuliwa katika Ziwa Victoria.
Alisema pamoja na kuendelea kuvua samaki, wananchi wanapaswa kutafuta njia za kuongeza thamani ya mazao hayo kupitia usindikaji, uhifadhi na biashara mbalimbali ili kuongeza kipato chao na kukuza uchumi wa eneo hilo.
Mkuu huyo wa Wilaya pia aliwahimiza wazazi na walezi kutumia mapato yatokanayo na shughuli za uvuvi kuwasomesha watoto wao ili wapate elimu bora itakayowawezesha kuwa wataalamu, viongozi na wafanyabiashara wa baadaye.
Aidha, aliwataka wananchi kuendelea kudumisha umoja, amani na usalama katika Kisiwa cha Gana na maeneo mengine ya Ukerewe, akisisitiza kuwa maendeleo hayawezi kupatikana bila kuwepo kwa mazingira ya utulivu na mshikamano.
Bw. Ngubiagai pia aliwahamasisha vijana na wanawake kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kutumia fursa ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Serikali kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye mahitaji maalum ili kuboresha maisha yao na ya familia zao.
Alisema Kisiwa cha Gana kina kila sababu ya kuwa mfano wa maendeleo katika Wilaya ya Ukerewe kutokana na uwepo wa rasilimali za Ziwa Victoria, nguvu kazi ya wananchi na mazingira ya amani, huku akitoa wito wa kufanya kazi kwa bidii, kulinda rasilimali zilizopo na kutumia vyema fursa za maendeleo zinazopatikana katika eneo hilo.

