Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma 

Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema kuwa hadi sasa Tanzania haina mgonjwa wa Ebola na hali ya usalama wa afya nchini inaendelea kuwa nzuri licha ya tishio la ugonjwa huo katika nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na Uganda.

Akizungumza na waandishi Juni 17,2026 Jijini Dodoma kuhusu mwenendo wa tishio la ugonjwa wa Ebola na hatua zinazoendelea kuchukuliwa ili kuzuia na kuimarisha utayari, Mchengerwa amesema kuwa Serikali imeendelea kuchukua hatua za mapema na za kina kuhakikisha ugonjwa huo hauingii nchini pamoja na kujiandaa kuzuia, kugundua mapema na kudhibiti tishio lolote la kiafya.Amesema kuwa kufuatia tishio hilo, Wizara ilitoa Mwongozo wa Wasafiri (Travel Advisory) Na. 17 wa tarehe 19 Mei, 2026 kwa wasafiri wote wanaoingia nchini ukiainisha hatua za kinga na udhibiti zinazopaswa kutekelezwa kwa mujibu wa Kanuni za Afya za Kimataifa na Sheria ya Afya ya Jamii.

Aidha, amebainisha kuwa Serikali imeimarisha ufuatiliaji wa tetesi katika jamii na uchunguzi wa afya kwa wasafiri wanaoingia nchini kupitia mipaka, bandari na viwanja vya ndege ili kubaini mapema viashiria vya ugonjwa huo.

Amesema kuwa hadi sasa jumla ya tetesi 64 kutoka mikoa 21 zimeripotiwa, ambapo wahisiwa 11 walikidhi vigezo vya uchunguzi, wakachukuliwa sampuli na baada ya kupimwa walithibitika kutokuwa na maambukizi ya Ebola.

Pia ameongeza kuwa Serikali imeimarisha utayari wa wataalam wa afya na vituo vya huduma kote nchini kwa kuhakikisha upatikanaji wa dawa, vifaa kinga na tiba muhimu ili kutoa huduma endapo ugonjwa huo utaingia nchini.

Waziri Mchengerwa amesema kuwa Serikali imehakikisha upatikanaji wa vifaa kinga maalumu, vifaa tiba na vifaa vingine muhimu kwa watoa huduma wa afya waliopo mstari wa mbele, huku seti za kutosha za vifaa hivyo zikiwa zimehifadhiwa katika Bohari ya Dawa (MSD) na mikoa yote kwa matumizi ya dharura.

Aidha, amebainisha kuwa Serikali imepeleka na kusimika maabara mbili jongezi zenye uwezo wa kupima sampuli za Ebola katika mikoa ya Kagera na Kigoma ili kusogeza huduma za upimaji karibu na wananchi wa maeneo yanayopakana na nchi zenye mlipuko.

Amesema kuwa Serikali imeendelea kujengea uwezo watoa huduma za afya nchini kupitia mafunzo ya ana kwa ana na ya mtandao ambapo jumla ya watoa huduma 45,000 wamefikiwa. Pia elimu ya kinga dhidi ya Ebola imeendelea kutolewa kwa wasafiri, watoa huduma na jamii za mipakani sambamba na uhamasishaji wa umma kupitia vyombo mbalimbali vya habari na mawasiliano.

Pia ameongeza kuwa tangu kutangazwa kwa mlipuko wa Ebola, jumla ya vyombo vya usafiri 101,302 vimekaguliwa na wasafiri 164,652 wamechunguzwa katika mipaka ya nchi kavu, viwanja vya ndege na bandari, wakiwemo raia 11,394 kutoka nchi zilizoathirika.

Amesema kuwa wasafiri 4,415 wa safari za kimataifa pia wamechunguzwa, ambapo 559 walitoka katika nchi zenye mlipuko, huku zoezi hilo likiendelea kuimarishwa katika mipaka na maeneo yote ya kuingilia nchini.

Aidha, amebainisha kuwa Tanzania inaendelea kushiriki kikamilifu katika juhudi za kikanda na za Bara la Afrika kupitia mikutano ya pamoja ya nchi wanachama wa Umoja wa Afrika na wadau wa afya ili kuimarisha uratibu wa afua za kudhibiti ugonjwa huo.

Pia ameongeza kuwa Serikali imeendelea kushirikiana na wizara za kisekta, mikoa, taasisi za umma na binafsi, viongozi wa dini, wananchi pamoja na wadau wa ndani na nje ya nchi katika kuimarisha afua za kuzuia Ebola.

Aidha amesema kuwa Serikali inaendelea kutoa taarifa za hali ya usalama wa afya nchini kwa mashirika ya kitaifa na kimataifa, wadau na balozi za nchi mbalimbali ili kuhakikisha Tanzania inaendelea kutambulika kama nchi salama kwa shughuli za kijamii, kiuchumi na utalii.

Pia, amewashauri wananchi kuendelea kuchukua tahadhari kwa kufuata kanuni za afya zilizotolewa na wataalam wa afya ikiwemo kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka na sabuni pamoja na kuzingatia usafi ili kujikinga dhidi ya magonjwa mengine ya kuambukiza.

Amesema kuwa Serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa ugonjwa huo na kuwajulisha wananchi mara kwa mara kuhusu hatua zinazochukuliwa, huku akiwataka wananchi kufuatilia taarifa kupitia vyanzo rasmi vya Serikali na kuepuka kueneza taarifa ambazo hazijathibitishwa.

Pia ameongeza kuwa mafanikio ya kuilinda Tanzania dhidi ya Ebola yanahitaji ushirikiano wa wananchi, viongozi wa jamii, taasisi za umma na binafsi pamoja na wadau wote wa maendeleo kwa kufuata maelekezo ya wataalam wa afya na kutoa taarifa mapema za wahisiwa.

Amebainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuimarisha uwekezaji katika mifumo ya afya, kuimarisha utayari wa taifa katika kuzuia, kugundua na kukabiliana na milipuko ya magonjwa pamoja na kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa taifa salama wakati wote.