*Awataka watendaji kuacha mazoea katika utekelezaji wa majukumu.
WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka watendaji wa Wizara ya Maji pamoja na Wakuu wa Mikoa wasimamie vizuri mitambo ya uchimbaji visima ili iweze kufanya kazi iliyokusudiwa.
Amesema Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alinunua mitambo ya uchimbaji wa visima hivyo watendaji wachukue hatua na waache kufanya kazi kwa mazoea.
“Nielekeze Wakuu wa Mikoa yote pamoja na wizara, kusimamia ili mitambo ile iweze kufanya kazi iliyokusudiwa, ni kweli kuna baadhi ya maeneo ya tunaendelea endelea na ile tabia ya _business as usual_, sasa ili kufikia matokeo ya Dira 2050, ni lazima tufanye kazi _business unusual_, tuache kufanya kazi kwa kuchukulia vitu kimazoea mazoea”, Ameelekeza Waziri Mkuu.
Dkt. Mwigulu ametoa maelekezo hayo leo (Alhamisi Juni 18, 2026) Bungeni jijini Dodoma katika kipindi cha Maswali kwa Waziri Mkuu wakati akijibu swali la Mbunge wa Kwimba, Cosmas Bullala.
Mbunge huyo alitaka kujua kauli ya Serikali kuhusu ufanisi wa mitambo hiyo, ambapo Mheshimiwa Dkt. Mwigulu amesema mitambo hiyo inaendelea kuchimba visima katika maeneo mbalimbali nchini. Ambapo kwa sasa unatekelezwa mpango wa uchimbaji visima 900.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu Mwigulu amesema Serikali inatarajia kuanza kuwalipa kifuta jasho askari waliojitolea katika vita dhidi ya Idd Amin wa Uganda mwaka 1978-79.
Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu ameeleza hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Njombe, Deodatus Mwanyika aliyetaka kujua ni lini Serikali itawalipa kifuta jasho askari hao, ambapo Waziri Mkuu Mwigulu amesema tayari Serikali imefanya mabadiliko ya Sheria ambapo sasa askari hao wanatambulika kisheria kutokana na hapo mwanzo kutotambuliwa.
“Mheshimiwa Spika, Sheria za zamani zilikuwa haziwatambui wapiganaji wale, hasa hasa wapiganaji waliopata mafunzo ya muda mfupi, hivi tunavyoongea, kupitia tangazo la Serikali la mwezi wa 6, mwaka 2025, kuhusu mabadiliko ya Sheria ya mafao ya veterani, sasa imeshawatambua wapiganaji hao”, Amesema Dkt. Mwigulu.
“Mheshimiwa Spika, wapiganaji hao wataanza kulipwa na watalipwa kwa kuwa sasa hakuna kikwazo cha kisheria ambacho kilikuwa kinawakwamisha, na kile cha uhakiki, kwani wapiganaji hao wameshahakikiwa”, Amesisitiza Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu.
