Na Silivia Amandius, Bukoba.
Bukoba: Walimu walioko kazini pamoja na vijana ambao hawakupata fursa ya kuendelea na elimu ya juu wametakiwa kutumia vyuo vinavyotoa mafunzo ya ujuzi kwa njia ya masafa ili kujiongezea maarifa na kujiandaa na utekelezaji wa mtaala mpya wa elimu unaolenga kukuza stadi na ujuzi wa kujitegemea.
Wito huo umetolewa katika mahafali ya nne ya wahitimu wa Chuo cha DC Polytechnic Education Institute College kilichopo Halmashauri ya Bukoba, ambapo wanafunzi 908 wamehitimu katika ngazi za shahada na astashahada kwenye fani mbalimbali zikiwemo ualimu, utawala, mawasiliano, teknolojia na ufundi.
Akizungumza katika kongamano la wahitimu wa chuo hicho, Mkurugenzi wa Huduma za Jamii kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. Elieth Lulu Niwagila, alisema maboresho ya mtaala wa elimu yanakusudia kuzalisha wahitimu wenye ujuzi, ubunifu na uwezo wa kutatua changamoto za jamii badala ya kutegemea maarifa ya darasani pekee.
Alisema wataalamu wa elimu wamejiridhisha na mwelekeo wa mtaala mpya unaoweka mkazo katika mafunzo ya stadi kwa kipindi cha miaka 10 ya elimu ya awali, hivyo walimu waliopo kazini wanapaswa kujiendeleza ili kuendana na mabadiliko hayo.
Meneja wa DC Polytechnic Education Institute College, Jackson Kailanga, alisema chuo hicho kinaendelea kutoa mafunzo kwa walimu na wananchi kwa njia inayowezesha hata waliopo kazini kuendelea na masomo huku wakitekeleza majukumu yao ya kila siku.
Aliongeza kuwa chuo hicho pia kinatoa mafunzo ya ufundi kwa vijana walioishia darasa la saba au kidato cha nne katika maeneo mbalimbali ikiwemo ufundi wa magari, umeme na stadi nyingine za kazi kwa ushirikiano na wataalamu kutoka VETA.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kanda ya Ziwa wa Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi (NACTVET), Godfrey Michael, aliwataka wahitimu kutumia elimu na ujuzi walioupata kuleta maendeleo katika jamii, kuzingatia maadili ya kazi na kuchangia mafanikio ya utekelezaji wa mtaala mpya wa elimu nchini.

