Na Mwandishi Wetu, WMJJWM Dar Es Salaam.
Waandishi wa habari na waandaaji wa vipindi vya watoto nchini wametakiwa kutumia vyombo vyao vya habari kuelimisha jamii kuhusu usalama wa watoto mtandaoni ili kukabiliana na ongezeko la vitendo vya ukatili na matumizi mabaya ya teknolojia yanayowaathiri watoto.
Wito huo umetolewa na Afisa wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari Tanzania, Prudence Constantine, alipokuwa akifungua mafunzo ya siku mbili kwa waandishi wa habari na waandaaji wa vipindi vya watoto kuhusu ulinzi na usalama wa mtoto mtandaoni yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Prudence amesema maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano yameleta manufaa makubwa katika upatikanaji wa taarifa, elimu, burudani na biashara, lakini pia yameongeza hatari mbalimbali zinazowakabili watoto wanapotumia mitandao bila uangalizi wa kutosha.
Amesema waandishi wa habari wana jukumu muhimu la kuelimisha wazazi, walezi na jamii kuhusu matumizi salama ya mtandao pamoja na madhara yanayoweza kuwapata watoto wanapotumia majukwaa mbalimbali ya kidijitali.
Akizungumzia hali halisi, Prudence amesema utafiti uliofanyika mwaka 2022 kwa watoto wenye umri wa miaka 12 hadi 17 ulibaini kuwa asilimia 67 ya watoto nchini wanatumia mtandao, huku mitandao maarufu ikijumuisha Facebook, Instagram, WhatsApp, TikTok na Telegram.
Amesema utafiti huo pia umeonesha kuwa baadhi ya watoto wamekumbana na aina mbalimbali za ukatili mtandaoni ikiwemo unyanyasaji, vitisho, ulaghai na kushawishiwa kutuma picha zisizofaa, hali inayohitaji hatua za haraka za kinga na elimu.
Kwa mujibu wa Prudence, Serikali imeendelea kuimarisha mifumo ya ulinzi wa mtoto kupitia marekebisho ya sheria mbalimbali ikiwemo Sheria ya Mtoto pamoja na utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto.
Awali, Afisa Huduma za Utangazaji kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Octavian Peter, amesema matumizi ya mitandao ya kijamii yamekuwa sehemu ya maisha ya kila siku ya watoto, jambo linalohitaji ushirikiano wa wadau wote katika kuhakikisha watoto wanatumia teknolojia kwa usalama
Amesema jukumu la kulinda watoto mtandaoni haliwezi kuachiwa serikali pekee, bali linahitaji ushirikiano wa wazazi, walezi, taasisi za elimu, wadau wa maendeleo pamoja na vyombo vya habari ambavyo vina nafasi kubwa ya kuelimisha umma.
Octavian amesema TCRA itaendelea kutekeleza jukumu lake la kusimamia sekta ya mawasiliano na utoaji wa maudhui kwa kuendelea kutoa elimu kwa umma na kushirikiana na wadau mbalimbali katika kukuza matumizi salama ya teknolojia.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa mafunzo hayo, Sabina Mpelo wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), amesema waandishi wa habari wana wajibu mkubwa katika kujenga kizazi chenye maadili na kinachotumia teknolojia kwa manufaa ya maendeleo ya taifa.
Sabina amesema mitandao ya kijamii inaweza kuwa nyenzo muhimu ya kujifunza na kupata taarifa, lakini pia inaweza kuwa chanzo cha madhara makubwa endapo haitatumika kwa uangalifu na usimamizi unaofaa.
Ametoa wito kwa washiriki wa mafunzo hayo kutumia maarifa watakayoyapata kuandaa maudhui yatakayosaidia kulinda watoto, kuhamasisha matumizi salama ya mtandao na kujenga jamii inayotambua haki na ustawi wa mtoto katika zama za kidijitali.

