Na Mwandishi Wetu
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF), imezuia kuanzia sasa watu kufika kwenye ofisi zake zilizopo Uwanja wa Karume Ilala Jijini Dar es Salaam na badala yake watakuwa wakihudumiwa kwa njia ya simu.
Taarifa ya TFF leo imesema kwamba wamechukua hatua hiyo kama sehemu ya tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa corona (COVID 19) unaoitikisa dunia kwa sasa.
“Ili kuwakinga wadau wa mpira wa miguu na maambukizi ya virusi vya corona, kuanzia leo Aprili 2, 2020 hadi itakapotangazwa vinginevyo. Sekretarieti ya TFF inawaomba wadau watumie mawasiliano ya simu na barua pepe na pale panapokuwa na ulazima ndipo wafike katika ofisi zetu kwa ajili ya kuhudumiwa,”imesema taarifa ya TFF leo.
Taarifa iliyosainiwa na Afisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Clifford Mario Ndimbo imeelekeza namba za mawasiliano kwa masuala mbalimbali zipo kwenye ukurasa wa Instagram wa shirikisho hilo.
Na hatua hiyo inakuja siku moja baada ya Mtendaji Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao kusema kwamba mustakabli wa msimu huu wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara utaamuliwa na vikao maalum iwapo janga la maambukizi ya virusi vya corona litaendelea.
Kidau alisema kwamba kama janga la COVID 19 litaendelea, msimu huu utategemea maamuzi yatakayofanywa na vyombo vinavyosimamia na kuendesha Ligi Kuu kwa pamoja na Kamati ya Utendaji ya TFF.
“Bado ni mapema sana kusema tumefuta msimu pamoja na kwamba msimu unaweza kwenda hadi Juni 31,” amesema Mtendaji Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao mapema leo alipozungumza na vyombo vya Habari Jijini Dar es Salaam.
Machi 17, mwaka huu TFF ilimesimamisha ligi zake zote ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufuatia mlipuko wa virusi vya ugonjwa wa corona duniani kote.
Pia TFF ilivunja kambi ya timu ya taifa, Taifa Stars iliyokuwa inajiandaa na fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) zilizopangwa kuanza Aprili 4 hadi 25, mwaka huu nchini Cameroon ambazo pia zimeahirishwa kwa sababu ya COVID 19.
Kwa ujumla CAF ilisimamisha mechi zote za kufuzu za mashindano ya Afrika kwa ushauri wa Shirika la Afya Dunani (WHO) kufuatia mlipuko wa virusi vya corona hadi hapo itakapaoamuliwa vinginevyo.
Ligi Kuu ilisimama huku Simba SC ikiwa inaongoza kwa pointi zake 71, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 54 baada ya timu zote kucheza mechi 28, wakati vigogo, Yanga SC ni wa tatu kwa pointi zao 51 za mechi 27 na Namungo wa nne wakiwa na pointi 50 za mechi 28.
Hali ni mbaya kwa Singida United inayoshika mkia kwa pointi zake 15 za mechi 29, nyuma ya Mbao FC pointi 22 mechi 28, Alliance FC pointi 29, mechi 29, Mbeya City pointi 30 mechi 29 na Ndanda FC pointi 31 mechi 29.