Na John Walter-Babati

Kwa miaka mingi, wakazi wa Tarafa ya Bashnet katika Wilaya ya Babati wameishi na changamoto ya kupata huduma za kipolisi kwa umbali mrefu.

Tarafa hiyo, inayojumuisha kata kumi za Bashnet, Nar, Dabil, Secheda, Madunga, Qameyu,Dareda,Arri,Ayalagaya na Ufana, imekuwa ikitegemea huduma za polisi kutoka Babati Mjini, hali iliyosababisha ucheleweshaji wa hatua za kiusalama na kuongeza gharama kwa wananchi wanaohitaji kuripoti matukio mbalimbali ya uhalifu.

Hata hivyo, hali hiyo inatarajiwa kuwa historia kufuatia ujenzi wa Kituo cha Polisi Bashnet unaoendelea kwa kasi na ambao umefikia asilimia 90 ya utekelezaji.

Mradi huo wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 110 unatajwa kuwa mkombozi wa usalama kwa maelfu ya wananchi wanaoishi katika eneo hilo muhimu kiuchumi.

Diwani wa Kata ya Bashnet, Jovitha Mandoo, anasema kwa sasa huduma za kipolisi katika tarafa hiyo zinapatikana kwa saa 12 pekee kutokana na changamoto ya ukosefu wa kituo kamili cha polisi chenye miundombinu inayohitajika.

Anasema askari waliopo eneo hilo hawana silaha kwa sababu hakuna sehemu rasmi ya kuhifadhi silaha hizo, jambo linalopunguza uwezo wao wa kukabiliana na vitendo vya uhalifu vinapotokea.

“Mahitaji ya kituo hiki ni makubwa sana. Askari waliopo hawana silaha kwa sababu hakuna sehemu ya kuzihifadhi. Hata ikitokea uhalifu, ni vigumu kuchukua hatua haraka. Ukiita polisi kutoka Babati, mara nyingi wahalifu huwa tayari wameondoka,” anasema Mandoo.

Anabainisha kuwa eneo la Mlima wa Dabil limekuwa likikumbwa na matukio ya utekaji wa magari na kuwahatarisha wafanyabiashara wanaosafirisha mazao na fedha, jambo linaloonesha umuhimu wa uwepo wa kituo hicho.

Tarafa ya Bashnet ni moja ya maeneo muhimu ya uzalishaji wa mazao ya biashara katika Mkoa wa Manyara.

Mazao kama vitunguu na mazao mengine ya kimkakati huzalishwa kwa wingi na kusafirishwa kwenda maeneo mbalimbali nchini.

Kutokana na shughuli hizo za kiuchumi, eneo hilo linavutia wafanyabiashara, mawakala wa huduma za kifedha pamoja na usafirishaji wa fedha taslimu, hali inayoongeza uhitaji wa ulinzi wa uhakika.

Kwa mujibu wa viongozi wa eneo hilo, kukamilika kwa kituo hicho kutasaidia kuimarisha usalama wa shughuli za kiuchumi na kuvutia uwekezaji zaidi katika sekta ya kilimo na biashara.

Mkazi wa Kijiji cha Bashnet, Regina Akko, anasema kwa sasa wananchi hulazimika kusafiri hadi Babati kufuata huduma za kipolisi, hali inayoongeza gharama na kupoteza muda.

“Kupatikana kwa kituo hiki kutatuondolea usumbufu mkubwa. Kwa sasa huduma nyingi za polisi tunazifuata Babati. Hii ni gharama kwa wananchi na wakati mwingine huchelewesha haki kupatikana,” anasema.

Kwa mujibu wake, uwepo wa kituo hicho karibu na wananchi utaongeza uharaka wa kushughulikia matukio na kuimarisha amani katika jamii.

Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mbunge wa Babati Vijijini, Mheshimiwa Daniel Sillo, ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho.

Akiwa eneo la mradi, Sillo amesema ujenzi wa kituo hicho umetokana na maombi ya muda mrefu ya wananchi waliotaka kusogezewa huduma za kipolisi karibu na maeneo yao.

Anasema kituo hicho kitasaidia kupunguza uhalifu, kurahisisha upatikanaji wa huduma za haki na usalama pamoja na kuongeza ufanisi wa Jeshi la Polisi katika Wilaya ya Babati.

“Hili ni ombi la wananchi wenyewe. Serikali imeendelea kusikiliza mahitaji yao na sasa tunashuhudia utekelezaji wake. Kukamilika kwa kituo hiki kutaleta mabadiliko makubwa katika masuala ya usalama na maendeleo ya wananchi,” amesema Sillo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Polisi Wilaya ya Babati,Mrakibu wa polisi (SP) Ernesta Mwambinga, anasema kituo hicho kitaongeza uwepo wa polisi karibu na wananchi na kuimarisha ulinzi wa raia na mali zao katika Tarafa ya Bashnet pamoja na maeneo jirani.

Anasema uwepo wa kituo hicho utawezesha askari kufanya kazi kwa ufanisi zaidi na kutoa huduma kwa wakati pale matukio ya kiusalama yanapotokea.

Mwenyekiti mstaafu wa Kijiji cha Bashnet, John Sulle, ambaye alishiriki katika mchakato wa kuanzishwa kwa mradi huo, anasema wananchi walikuwa mstari wa mbele kuomba kituo hicho kwa miaka mingi.

Anasema sababu kubwa ilikuwa ni kuepuka safari ndefu za kwenda kuripoti matukio ya uvunjifu wa amani na vitendo vingine vya uhalifu.

Kwa kutambua umuhimu wa huduma hiyo, kijiji kilitoa eneo lenye ukubwa wa robo tatu kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho.

“Wananchi walikuwa wanahitaji sana kituo hiki. Tulitoa eneo la kijiji kwa hiari kwa sababu tuliona usalama ni msingi wa maendeleo. Kikiwepo kituo hiki, hata wahalifu wataogopa kufanya vitendo vyao kwa kuwa watakuwa wanajua polisi wako karibu,” anasema Sulle.

Anaongeza kuwa uwepo wa kituo hicho utasaidia kupunguza vitendo vya ukatili na uhalifu kwa sababu watuhumiwa watakuwa wanakamatwa kwa haraka zaidi.

Pamoja na matumaini makubwa ya kukamilika kwa mradi huo, viongozi na wananchi wa Bashnet wanaendelea kuiomba Serikali kuhakikisha kituo hicho kinakamilika haraka na kuwezeshwa kwa vifaa muhimu vya kazi, ikiwemo gari la doria.

Kwa mujibu wao, uwepo wa gari la doria utasaidia kufikia maeneo mbalimbali ya tarafa kwa haraka zaidi na kuongeza ufanisi wa kazi za ulinzi na usalama.

Kadiri ujenzi wa Kituo cha Polisi Bashnet unavyokaribia kukamilika, ndivyo matumaini ya wananchi yanavyozidi kuongezeka.

Kwa eneo ambalo ni kitovu cha uzalishaji wa mazao ya biashara na shughuli mbalimbali za kiuchumi, uwekezaji katika usalama unatajwa kuwa hatua muhimu ya kulinda maendeleo yaliyopo na kufungua milango ya fursa mpya.

Kwa wakazi wa Bashnet na kata jirani, kituo hicho si jengo la kawaida bali ni alama ya usikivu wa Serikali kwa mahitaji ya wananchi, hatua inayotarajiwa kuimarisha amani, usalama na maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa miaka mingi ijayo.