NA DENIS MLOWE IRINGA
MBUNGE wa Jimbo la Kalenga, Jackson Kiswaga, ameendelea kuonyesha dhamira yake ya kusimamia maendeleo ya wananchi kwa kuibana Serikali kuhusu hatima ya ujenzi wa barabara ya Ifunda–Kiponzero yenye urefu wa kilomita 12, ambayo ni muhimu kwa shughuli za kiuchumi na kijamii katika eneo hilo.
Akiuliza swali la nyongeza bungeni, Mheshimiwa Kiswaga alisema barabara hiyo ni kiungo muhimu kinachorahisisha usafirishaji wa watu na bidhaa katika maeneo ya Ifunda na Kiponzero, hivyo alihoji ni lini Serikali itaona umuhimu wa kuijenga kwa kiwango cha lami ili kuongeza kasi ya maendeleo ya uchumi kwa wananchi wa Kalenga.
“Barabara ya kutoka Ifunda kwenda Kiponzero ni barabara muhimu sana ya kiuchumi. Je, ni lini sasa Serikali, maana ni kilomita 12 tu, itaona umuhimu wa kutujengea kwa lami ili tuendelee kuchagiza shughuli za kiuchumi zinazofanyika katika eneo hilo?” alihoji Mbunge huyo.
Akijibu swali hilo kwa niaba ya Serikali,Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) nchini Tanzania. Dokta Festo John Dugange
alikiri umuhimu wa barabara hiyo na kueleza kuwa ni miongoni mwa barabara kongwe zinazohudumia wananchi kwa muda mrefu katika Jimbo la Kalenga.
Alisema Serikali inaendelea kutekeleza mkakati wa kuboresha miundombinu ya barabara nchini kwa awamu mbalimbali, ambapo baadhi ya barabara zinajengwa kwa kiwango cha udongo, nyingine changarawe na zile zenye umuhimu mkubwa zaidi hujengwa kwa kiwango cha lami.
“Dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kwamba kwa awamu mbalimbali barabara za udongo zinahamia kiwango cha changarawe na zile za changarawe ambazo ni muhimu sana zinajengwa kwa kiwango cha lami,” alisema Naibu Waziri.
Aidha, Serikali ilimhakikishia Mbunge huyo pamoja na wananchi wa Kalenga kuwa barabara ya Ifunda–Kiponzero itaendelea kufanyiwa tathmini kulingana na upatikanaji wa fedha katika bajeti za Serikali, ikiwa ni hatua muhimu kuelekea kuanza kwa mchakato wa ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami siku zijazo
Hatua ya Mbunge Jackson Kiswaga kuendelea kuwasilisha mahitaji ya wananchi wake bungeni inaonesha jitihada zake za kutafuta suluhisho la changamoto za miundombinu zinazokwamisha ukuaji wa shughuli za kilimo, biashara na huduma za kijamii katika Jimbo la Kalenga.
Wananchi wa maeneo ya Ifunda na Kiponzero wana matumaini kuwa msukumo unaotolewa na mwakilishi wao bungeni utasaidia kuharakisha utekelezaji wa mradi huo muhimu, ambao unatarajiwa kufungua zaidi fursa za kiuchumi na kuboresha maisha ya wananchi wa eneo hilo.
