Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kushirikiana na wananchi na wadau wengine katika kuimarisha ulinzi na usalama wa maisha na mali kwa kufanya doria za kubaini na kuzuia uhalifu. Pia oparesheni na misako imeendelea kufanyika na kufanikiwa kuwakamata wahalifu wa makosa mbalimbali.
MTOTO ALIYETEKWA APATIKANA KATIKATI YA HIFADHI YA KITULO
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kupitia kikosi maalum cha kuzuia na kupambana na uhalifu limefanikiwa kumpata mtoto Razaki Damas Mwakatundu, miaka 05, Mwananfunzi wa Chekechea katika Shule ya Mwakikome iliyopo Wilaya ya Kyela aliyekuwa ametekwa na mtu aliyetajwa kuwa ni baba yake mlezi.
Ni kwamba Juni 1, 2026 katika maeneo ya Kata ya Katumbasongwe Wilayani Kyela, Mkoa wa Mbeya mtoto huyu akiwa anacheza na wenzake nyumbani kwao alifika baba mlezi na kumchukua na kuondoka naye na kwenda kusikojulikana huku akishinikiza kurudishiwa kiasi cha pesa shilingi 550,000/= alichotoa kama mahari ya kumuoa mama wa mtoto baada ya mama huyo kukataa kuolewa baada ya kupokea kiasi hicho cha fedha.
Baada ya taarifa kutolewa Polisi na kesi kufunguliwa ndipo msako mkali ulianza ndipo Juni 14, 2026 mtoto huyo alipatikana akiwa hai akiwa ametelekezwa katikati ya msitu wa hifadhi ya Kitulo uliopo mpakani mwa Mbeya na Njombe.
Msako mkali unaendelea kumtafuta mtuhumiwa ambaye alimteka na kisha kumtelekeza mtoto huyo baada ya kubaini anafuatiliwa na Polisi.
AKAMATWA AKISAFIRISHA DAWA ZA KULEVYA KWENYE BASI LA ABIRIA.
Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Idd Hussein Robert, Mkazi wa Kimara Dar es Salaam kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya aina ya Bhangi yenye uzito wa kilo 30.
Mtuhumiwa alikamatwa Juni 14, 2026 saa 1:30 usiku huko katika kizuizi cha Polisi (Police Check Point) kiitwacho Mafiga kilichopo Kata ya Busare, Tarafa ya Unyakyusa, Wilayani Kyela akiwa anasafirisha dawa hizo za kulevya aina ya Bhangi vifurushi 13 vyenye uzito kilogram 30 vilivyokuwa vimehifadhiwa ndani ya begi kubwa la nguo la plastiki na begi la mgongoni.
Mtuhumiwa alikuwa akisafirisha dawa hizo katika basi akitokea Kyela kuelekea Dar es Salaam. Uchunguzi wa awali umebaini kuwa mtuhumiwa ni msafirishaji na muuzaji wa dawa hizo.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa wazazi kutumia njia sahihi kutatua migogoro kwa njia sahihi badala ya kuwahusisha watoto kwa kuwatendea ukatili kama ilivyofanyika kwa mtoto huyo alitekwa na kwenda kutelekezwa kwenye msitu wa Kitulo. Pia, Jeshi la Polisi linaendelea kutoa rai kwa baadhi ya wananchi wenye tamaa ya kujipatia fedha kwa njia zisizo halali kuacha mara moja na badala yake wafanye shughuli halali ili kuepuka kuingia kwenye mgogoro na sheria za nchi na matokeo yake ni kuharibu maisha yao ya baadae.

