Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Serikali itaendelea kulinda uhuru wa kuabudu na kuimarisha ushirikiano na taasisi za dini kwa kutambua mchango mkubwa unaotolewa na taasisi hizo katika kujenga maadili, amani, mshikamano na maendeleo ya Taifa.

Dkt. Mwigulu amesema hayo leo, Jumapili Juni 14, 2026, aliposhiriki Ibada katika Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) Kiomboi Christian Centre, mjini Kiomboi, Wilaya ya Iramba mkoani Singida.

Ibada hiyo iliongozwa na Askofu wa Jimbo la Singida Kaskazini, Dkt. Danford Obadia pamoja na Mchungaji Kiongozi wa Kanisa hilo, Yona Suleman Essya.

Akizungumza na waumini hao, Waziri Mkuu amesema Serikali inatambua nafasi muhimu ya taasisi za dini katika malezi ya jamii na kwamba itaendelea kuweka mazingira rafiki yatakayowezesha taasisi hizo kutekeleza majukumu yake kwa uhuru na ufanisi.

“Sisi wote tutaendelea kulinda mazingira bora ya kuendesha ibada. Serikali itaendelea kutambua na kuamini kazi inayofanywa na taasisi za dini katika kujenga Taifa letu,” amesema Dkt. Mwigulu.

Amesema taasisi za dini zimekuwa mshirika muhimu wa Serikali katika kujenga maadili mema, kuhimiza uwajibikaji, kuimarisha mshikamano wa kijamii na kupambana na vitendo vinavyokinzana na utu na maendeleo ya wananchi.

Waziri Mkuu amesema Kanisa la TAG limekuwa na mchango mkubwa katika kuelimisha jamii, kuondoa imani potofu na kuhamasisha wananchi kuzingatia maadili na misingi sahihi ya maisha.

“TAG haikusimama kwenye ibada pekee, bali imebadilisha hata maisha ya kila siku ya wananchi. Imechangia kuondoa baadhi ya mila na imani zilizokuwa zinarudisha nyuma maendeleo ya watu wetu,” amesema.

Wakati huo huo, Dkt. Mwigulu ametoa rai kwa wananchi kuendelea kuheshimu nyumba za ibada na kuepuka kuziingiza katika shughuli zinazoweza kuvuruga dhamira na malengo yake ya msingi.

“Ukitaka siasa anzisha chama cha siasa. Usipeleke fujo kwenye nyumba ya ibada. Lazima tuendelee kuheshimu utakatifu wa nyumba zetu za ibada,” amesema.

Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali itaendelea kupokea ushauri na maoni kutoka kwa viongozi wa dini ili kuboresha zaidi mazingira ya utoaji huduma kwa wananchi na kuimarisha maendeleo ya Taifa.

Awali akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na waumini, Askofu wa Jimbo la Singida Kaskazini, Dkt. Danford Obadia amesema kanisa linaendelea kumuombea Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na viongozi wa Serikali ili waendelee kutekeleza majukumu yao kwa hekima, uadilifu na mafanikio kwa manufaa ya Taifa.

Askofu Obadia amesema Watanzania wana wajibu wa kuliombea Taifa na viongozi wake kwa mujibu wa mafundisho ya Biblia ili nchi iendelee kudumisha amani, utulivu na maendeleo.

“Kabla ya mambo yote, nataka dua na sala na maombezi yafanyike kwa ajili ya wafalme na wenye mamlaka, ili tuweze kuishi kwa amani na utulivu. Hii nchi ni ya kwetu; tukiipenda nchi yetu na kuwaombea viongozi wetu, tutakaa nchi hii salama na tutaondoka duniani salama,” amesema Askofu Obadia.