Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Dodoma
Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar, amesema Bajeti ya Serikali ya mwaka 2026/27 ni ya kipekee kwani ndiyo bajeti ya kwanza kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2026/27–2030/31) pamoja na Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma Juni 10, 2026 katika kikao cha kutoa dondoo za bajeti kabla ya kuiwasilisha rasmi bungeni kesho, Waziri Omar amesema Serikali inatarajia kutumia jumla ya Shilingi trilioni 62.3 katika mwaka wa fedha 2026/27, huku sehemu kubwa ya fedha hizo ikitarajiwa kugharamiwa na mapato ya ndani yatakayofikia Shilingi trilioni 46.8.
Amesema Kuwa Serikali itaendelea kuweka mkazo katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), barabara, miradi ya maji, nishati pamoja na uwekezaji katika rasilimali watu na maendeleo ya ujuzi.
Waziri Omar amesema utekelezaji wa Bajeti ya mwaka 2025/26 umeonyesha mafanikio makubwa kutokana na ukusanyaji mzuri wa mapato ya ndani ambao umewezesha kufikiwa kwa malengo yaliyowekwa na Serikali.
Aidha, amebainisha kuwa katika maandalizi ya bajeti mpya, Serikali ilipokea mapendekezo 727 kutoka kwa wadau mbalimbali kuhusu maboresho ya kodi, ada na tozo, ambapo mapendekezo 125 yalikubaliwa moja kwa moja huku mengine yakifanyiwa maboresho au kupelekwa kwa taasisi husika kwa uchambuzi zaidi.
Ameeleza kuwa mapendekezo hayo yalichambuliwa na Kamati ya Wataalam wa Maboresho ya Kodi pamoja na Kamati ya Kiufundi ya Ngazi ya Juu (Think Tank), yenye wajumbe kutoka Serikalini, sekta binafsi na taasisi za utafiti, kabla ya kufanyiwa maamuzi ya mwisho.
Waziri Omar amesema ushirikishwaji wa wadau katika mchakato wa maboresho ya kodi umeendelea kuimarishwa kwa lengo la kukuza uchumi, kuvutia uwekezaji, kuongeza ajira na kupunguza mzigo wa kodi kwa walipakodi.
Aidha, amewataka Watanzania kuendelea kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi kwa hiari na kwa wakati, huku Serikali ikiendelea kuimarisha usimamizi wa matumizi ya fedha za umma ili kuhakikisha zinatumika kwa ufanisi na kuleta maendeleo kwa wananchi.
Mhe. Omar anatarajiwa kuwasilisha rasmi Bajeti ya Serikali ya mwaka 2026/27 mbele ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kesho Juni 11, 2026.
