Dodoma.
Bohari ya Dawa (MSD) imeihakikishia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI kuwa itaendelea kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya zenye ubora, kwa wakati na kwa kiwango kinachohitajika kuelekea utekelezaji wa awamu ya pili ya Bima ya Afya kwa Wote.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai, mbele ya Kamati hiyo Juni 9, 2026 mara baada ya wajumbe wa Kamati hiyo kufanya ziara katika Ghala Kuu la MSD Dodoma kwa lengo la kujionea shughuli za kila siku za taasisi hiyo katika uzalishaji, ununuzi, uhifadhi na usambazaji wa bidhaa za afya.
“Sisi tumeshajipanga, na utayari wetu unategemea kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa rasilimali. Tayari tumewasilisha mahitaji yetu Serikalini kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote na kuhakikisha wananchi wanapata huduma zinazostahili,” amesema Mavere.
Amesema MSD inaendelea kujiandaa kukidhi ongezeko la mahitaji ya bidhaa za afya litakalotokana na utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote, huku akibainisha kuwa bidhaa za afya zenye thamani ya zaidi ya Shilingi trilioni 1.2 hununuliwa kupitia MSD na kusambazwa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.
Katika ziara hiyo, wajumbe wa Kamati walipata maelezo kuhusu mifumo ya ugavi wa bidhaa za afya, hatua zinazochukuliwa kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa hizo nchini pamoja na mifumo ya udhibiti wa ubora inayotekelezwa kwa kushirikiana na mamlaka mbalimbali ikiwemo Mamlaka ya Dawa na VifaaTiba (TMDA) na taasisi nyingine za ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Mhe. Johannes Lukumay, ameipongeza MSD kwa kazi kubwa inayofanya ya kuhakikisha wananchi wanapata bidhaa za afya zenye ubora na kwa wakati, huku akiitaka taasisi hiyo kuendelea kuimarisha mifumo yake ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya huduma za afya nchini.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Dkt. Zeyana Abdallah Hamid, ameutaka uongozi wa MSD kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu shughuli za taasisi hiyo ili wananchi waweze kufahamu thamani ya uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika kuhakikisha bidhaa za afya zinapatikana kwa uhakika nchini.

