NA FAUZIA MUSSA

MKURUGENZI wa Kampuni ya DeepSearch International Ltd, Yussuf Washokera, amesema kuanzishwa kwa mfumo rasmi wa kidijitali unaowaunganisha madereva na waajiri kutasaidia madereva kupata ajira kwa haraka huku ukiondoa changamoto ya kutokuwa na taarifa sahihi za wataalamu hao wa usafirishaji.

Washokera alieleza hayo wakati wa uzinduzi wa jukwaa la DrivingLink Africa uliofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip Airport, Zanzibar, akisema tafiti zilizofanywa na kampuni hiyo zimebaini kuwa zaidi ya asilimia 80 ya madereva hawapo katika mifumo rasmi ya ajira, hali inayochangia ugumu wa kupata kazi na kuathiri maendeleo ya sekta ya usafirishaji.

Alisema ndani ya kipindi cha miezi miwili tangu mfumo huo uzinduliwe Tanzania Bara mwezi Aprili mwaka huu, madereva 1,503 pamoja na kampuni 62 za usafirishaji tayari wamejisajili na kuanza kutumia huduma zake.

“Leo tunaufikisha mfumo huu Zanzibar ili uweze kuwahudumia madereva na waajiri kwa njia ya kisasa zaidi. Ndani ya miaka mitatu ijayo tunatarajia madereva wengi Afrika watakuwa kwenye mfumo rasmi wa kidijitali kama ilivyo kwa huduma nyingine mbalimbali,” alisema Washokera.

Alifafanua kuwa kampuni zitakazojisajili katika mfumo huo zitanufaika kwa kupata madereva bila gharama za mawakala, jambo litakalowezesha kuokoa kati ya asilimia 15 hadi 30 ya gharama za uajiri.

Aidha, mfumo huo utatoa hifadhidata ya madereva waliothibitishwa, kupunguza udanganyifu na kusaidia kuzuia ajira za madereva wenye historia ya utendaji usioridhisha.

Kwa upande wa madereva, alisema mfumo huo utawapa fursa ya kuingia moja kwa moja katika soko la ajira la Afrika, kupunguza muda wa kutafuta kazi kwa kati ya asilimia 40 hadi 60, pamoja na kuwawezesha kupata taarifa za nafasi za kazi ndani na nje ya Tanzania.

Washokera alieleza kuwa kada zote za udereva zitapatikana katika jukwaa hilo, hatua itakayorahisisha upatikanaji wa ajira na kuongeza uwazi katika sekta ya usafirishaji.

Mbali na kuwa daraja la ajira, alisema mfumo huo unatarajiwa kuongeza ajira za madereva kwa kati ya asilimia 50 hadi 70, kupunguza wizi wa mizigo kwa asilimia 30 hadi 40 na kuongeza kipato cha madereva kwa kati ya asilimia 15 hadi 25.

“DrivingLink Africa italeta mapinduzi makubwa katika mlolongo wa usafirishaji barani Afrika kwa kuwaunganisha madereva, kampuni za usafirishaji na taasisi mbalimbali kupitia mfumo mmoja wa kisasa,” alisema.

Naye Ofisa Masoko wa DeepSearch International Ltd, Trevor Steven, alisema mfumo huo umeundwa kusaidia kampuni na taasisi mbalimbali kuajiri na kusimamia madereva kwa ufanisi zaidi huku ukiwapa madereva nafasi ya kupata ajira ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.

Alisema kupitia programu ya DrivingLink Africa App, madereva watajisajili na kuweka taarifa zao muhimu zitakazowezesha waajiri kuwafikia kwa urahisi.

Aidha, mfumo huo utasaidia kutambua madereva wenye utendaji duni au wanaosababisha hasara kwa waajiri kupitia mfumo wa tathmini na orodha maalumu ya waendeshaji wasiozingatia maadili ya kazi.

“Kwa sasa dereva anaweza kuondoka kampuni moja kwenda nyingine bila mwajiri mpya kujua sababu za kuondoka kwake. Mfumo huu utasaidia kuweka wazi historia ya utendaji wake na kuongeza uwajibikaji,” alisema Steven.

Aliongeza kuwa kampuni yoyote itakayojisajili itaweza kuona taarifa za madereva, sifa zao, uzoefu wao na vielelezo mbalimbali vinavyohitajika katika mchakato wa ajira. Vilevile, madereva wataweza kuona nafasi za kazi zilizopo, aina ya madereva wanaohitajika pamoja na viwango vya mishahara vinavyotolewa.

Kwa upande wao, baadhi ya washiriki wa hafla hiyo waliitaka kampuni hiyo kushirikiana kwa karibu na Serikali pamoja na taasisi za usafiri ili kuhakikisha madereva wengi wanajiunga na mfumo huo na kunufaika na fursa zake.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani, Fadhil Ali, alisema jukwaa hilo litasaidia kujenga hadhi ya taaluma ya udereva na kuongeza heshima ya madereva katika jamii.

Alisisitiza umuhimu wa kufanya vikao vya pamoja kati ya wadau wa sekta ya usafirishaji na mamlaka husika ili kuweka mikakati madhubuti ya kufanikisha matumizi ya teknolojia ya kidijitali katika sekta hiyo.

Naye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Jumuiya ya Waongoza Watalii Zanzibar (ZATO), Raya Juma Omar, alisema mfumo huo utasaidia kupunguza vitendo vya wizi na uhalifu vinavyoweza kufanywa na baadhi ya madereva wasiokuwa waaminifu huku ukiwawezesha madereva kupata fursa zaidi za ajira.

Alisema sekta ya utalii itanufaika kwa kupata madereva salama, wanaotambulika na wenye taarifa zinazoweza kuthibitishwa kwa urahisi.

Baadhi ya madereva waliozungumza nje ya uzinduzi huo walieleza matumaini yao makubwa juu ya mfumo huo.

Abdalla Mussa Abdalla, mmoja wa madereva hao, alisema DrivingLink Africa inaweza kuwa kituo muhimu cha kukuza ufanisi, uwazi na uaminifu katika sekta ya usafirishaji iwapo itatumika kwa usahihi.

Programu ya DrivingLink Africa imebuniwa kwa lengo la kurahisisha na kubadilisha namna ya kuwaunganisha madereva wataalamu, kampuni za usafirishaji na taasisi mbalimbali katika nchi zote 54 za Afrika, hatua inayotarajiwa kuleta mageuzi makubwa katika ajira na usimamizi wa rasilimali watu katika sekta ya usafiri.