Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza S. Johari. 

………….

Na John Bukuku, Dar es Salaam

Kwa miaka mingi, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ilikuwa ikitazamwa zaidi kama taasisi ya ushauri wa kisheria serikalini. Lakini katika kipindi cha hivi karibuni, ofisi hiyo imebadilika na kuwa mhimili muhimu katika utekelezaji wa diplomasia ya uchumi ya Tanzania, hasa katika kusimamia mikataba ya uwekezaji, kulinda rasilimali za taifa na kuhakikisha maslahi mapana ya nchi yanazingatiwa katika majadiliano ya kimataifa.

Tangu alipoteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali mwezi Agosti mwaka 2024, Hamza S. Johari ameonekana kuipa ofisi hiyo sura mpya ya kiutendaji na kimkakati. Chini ya uongozi wake pamoja na Menejimenti Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imekuwa mstari wa mbele katika uchambuzi, majadiliano na usimamizi wa mikataba yenye maslahi makubwa kwa taifa.

Takwimu zinaonesha kuwa katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, ofisi hiyo ilifanya upekuzi wa mikataba 2,562 ya kitaifa, kikanda na kimataifa pamoja na kupitia Hati za Makubaliano 396. Aidha, ilisimamia mikataba 2,821 iliyosainiwa kati ya Serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo na uwekezaji.

Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Samwel M. Maneno. 

Kwa tafsiri ya kawaida, hizi ni namba tu. Lakini kwa jicho la uchambuzi wa kiuchumi na kisera, takwimu hizo zinaakisi namna ambavyo Tanzania imeamua kuingia katika ushindani wa uchumi wa dunia kwa kutumia sheria kama nyenzo ya kulinda rasilimali na maslahi ya wananchi wake.

Katika dunia ya sasa, vita vya kiuchumi havipiganwi kwa kutumia silaha, bali kupitia vifungu vya mikataba, sheria za biashara, usimamizi wa uwekezaji na uwezo wa nchi kujadiliana kwa manufaa yake. Taifa lisipokuwa na wataalamu wenye uwezo wa kuchambua mikataba kwa umakini, linaweza kupoteza mapato, rasilimali na hata uhuru wa maamuzi ya kiuchumi kwa miaka mingi ijayo.

Ndiyo maana hatua ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuimarisha uwezo wa mawakili wa serikali katika majadiliano ya mikataba ya uwekezaji na biashara ni jambo la kimkakati kwa mustakabali wa taifa.

Bw. Onorius John Njole Mwandishi Mkuu wa Sheria. 

Mwaka 2025, ofisi hiyo iliendesha mafunzo maalumu jijini Arusha kwa mawakili wa serikali kuhusu mbinu za majadiliano ya mikataba ya uwekezaji, biashara na usimamizi wa migogoro ya kimataifa. Mafunzo hayo yalilenga kuwajengea uwezo mawakili hao katika maeneo ya usuluhishi wa migogoro ya uwekezaji, tafsiri ya mikataba ya kimataifa na namna ya kuhakikisha Tanzania inanufaika ipasavyo na uwekezaji unaoingia nchini.

Sasa juhudi hizo zinaendelea kupewa nguvu mpya kupitia Mafunzo ya Tatu ya Mwaka ya Bespoke kwa Mawakili wa Serikali yatakayofanyika kuanzia Juni 22 hadi 24, 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha AICC jijini Arusha. Mafunzo hayo yamebeba kaulimbiu isemayo; “Kumuweka Wakili wa Serikali katika Nafasi ya Uongozi wa Sheria wa Kimkakati katika Kufikia Malengo ya Dira ya Taifa 2050.”

Mwanasheria Mkuu wa Serikali  Mhe. Hamza S. Johari akiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. 

Kaulimbiu hiyo pekee inaonesha namna Serikali ilivyoanza kuiona taaluma ya sheria kama nyenzo muhimu ya kufanikisha maendeleo ya taifa. Hii ni kwa sababu utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050 hautahitaji uwekezaji pekee, bali utahitaji wataalamu wa sheria wenye uwezo wa kusimamia mikataba mikubwa ya kimkakati, kulinda rasilimali za taifa na kuhakikisha Tanzania inanufaika katika ushindani wa uchumi wa dunia.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kujadili nafasi ya mawakili wa serikali katika kuimarisha diplomasia ya uchumi, usimamizi wa mikataba ya uwekezaji, biashara ya kimataifa na ulinzi wa maslahi ya taifa katika miradi ya maendeleo. Aidha, yataongeza uwezo wa mawakili wa serikali kwenda sambamba na kasi ya mabadiliko ya sheria za biashara, uwekezaji na usuluhishi wa migogoro ya kimataifa.

Baada ya mafunzo hayo, Juni 26, 2026, kutafanyika kikao kazi maalumu kitakachomkutanisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Wakurugenzi, Wakuu wa Idara, Divisheni pamoja na Vitengo vya Huduma za Sheria Serikalini. Kikao hicho kinatarajiwa kuwa sehemu ya tathmini ya utekelezaji wa majukumu ya sheria serikalini pamoja na kuweka mikakati mipya ya kuimarisha utendaji wa huduma za sheria katika taasisi za umma.

Kwa ujumla, hatua hizi zinaashiria mabadiliko makubwa ya kimtazamo ndani ya Serikali kuhusu nafasi ya sheria katika maendeleo ya taifa. Leo hii, mwanasheria wa serikali haonekani tena kama mtendaji wa kawaida wa sheria, bali kama mlinzi wa uchumi wa taifa, mshauri wa kimkakati wa Serikali na sehemu ya mfumo wa diplomasia ya uchumi wa Tanzania.

Katika kipindi ambacho ushindani wa kiuchumi duniani unaongezeka kila siku, Tanzania haihitaji tu wawekezaji wengi, bali inahitaji mikataba bora yenye manufaa ya muda mrefu kwa wananchi wake. Na katika safari hiyo, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inaendelea kujijenga kama moja ya taasisi muhimu zinazobeba matumaini ya kulinda maslahi mapana ya taifa.