Na Silivia AmandiusÂ
Muleba,Kagera.
Mashindano ya soka kwa vijana ya Kamachumu Paul Mwijage Cup yamezinduliwa rasmi katika Tarafa ya Kamachumu, Wilaya ya Muleba mkoani Kagera, yakishirikisha timu 20 zinazowania zawadi ya shilingi milioni 6 kwa lengo la kuibua vipaji na kukuza maendeleo ya michezo katika jamii.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mashindano hayo uliofanyika Juni 7 katika Uwanja wa Polisi Kamachumu, Ndg. Paul Mwijage, amesema kuwa ligi hiyo inapaswa kuwa desturi ya kuwakutanisha vijana mara kwa mara ili pamoja na michezo waweze kujadili masuala mbalimbali ya maendeleo yanayowahusu.
Mwijage amesema kuwa mashindano hayo ni sehemu ya utekelezaji wa malengo ya taasisi yake ya Mwijage Compassion and Development Foundation, ambayo inalenga kuanzisha akademi za michezo zitakazosaidia kukuza vipaji vya vijana. Ameeleza kuwa kuanzia Kamachumu ni hatua ya kuwapa nafasi vijana wenye umri chini ya miaka 20 kuonesha uwezo wao na kufungua fursa za maendeleo kupitia michezo.
Aidha, amesema ana matumaini kuwa mashindano hayo yatakuwa na mwendelezo wa muda mrefu, hata kwa kipindi cha miaka 10 ijayo, huku yakichangia kuifanya Kamachumu kuwa kitovu cha michezo na uchumi wa vijana tofauti na maeneo mengine ya mkoa wa Kagera.
Kwa upande wake, mgeni rasmi katika uzinduzi huo ambaye pia ni Msemaji wa Klabu ya Simba SC, Ahmed Ally, amempongeza Mwijage kwa kuanzisha mashindano hayo akisema yamekuwa chachu muhimu ya kuwaunganisha vijana na kuwapa fursa ya kuonesha vipaji vyao mbele ya wadau wa soka.
Ahmed Ally amewahimiza vijana wanaoshiriki mashindano hayo kutumia jukwaa hilo kuonesha uwezo wao wa kisoka, akibainisha kuwa mashindano ya ngazi ya jamii yamekuwa chanzo kikubwa cha kuibua vipaji vinavyochezea klabu mbalimbali nchini, ikiwemo Simba SC, huku akiwataka kutokata tamaa katika kufuatilia ndoto zao za mafanikio kupitia michezo.

