Rais wa Jamhuri ya Singapore, Mheshimiwa Tharman Shanmugaratnam, anatarajiwa kuwasili nchini leo jioni kwa ziara ya kitaifa kufuatia mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bakari S. Machumu, Rais Shanmugaratnam atapokelewa rasmi kesho, Juni 9, 2026, Ikulu jijini Dar es Salaam na mwenyeji wake Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Viongozi hao wawili wanatarajiwa kufanya mazungumzo rasmi yatakayolenga kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Singapore katika sekta mbalimbali ikiwemo biashara, uwekezaji, maendeleo ya rasilimali watu na ujuzi pamoja na uchumi wa kidijitali.

Baada ya mazungumzo hayo, viongozi hao watashuhudia utiaji saini wa mikataba na hati za ushirikiano kati ya nchi hizo mbili kabla ya kufanya mkutano wa pamoja na waandishi wa habari.

Aidha, Rais Shanmugaratnam akiambatana na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan atashiriki Jukwaa la Wafanyabiashara wa Tanzania na Singapore litakalofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.

Jukwaa hilo linatarajiwa kuwakutanisha viongozi wa sekta ya umma na binafsi kutoka Tanzania na Singapore kwa lengo la kujadili fursa mpya za biashara, uwekezaji na ushirikiano wa kiuchumi.

Katika ziara hiyo, Rais Shanmugaratnam pia atahutubia mhadhara wa wazi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wenye mada ya “Uwekezaji katika Vichocheo vya Ukuaji Jumuishi,” ambapo atazungumzia uzoefu wa Singapore katika kujenga uchumi shindani unaojumuisha wananchi wote.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa Juni 10, 2026, Rais Shanmugaratnam atafanya ziara Zanzibar na kufanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, kabla ya kurejea Dar es Salaam na kuondoka nchini baada ya kuhitimisha ziara yake.

Kwa mujibu wa Ikulu, ziara hiyo inaashiria hatua muhimu katika kuimarisha uhusiano wa muda mrefu wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Singapore pamoja na kufungua fursa mpya za ushirikiano wa kiuchumi, biashara, uwekezaji, maendeleo ya ujuzi na ubadilishanaji wa uzoefu katika maeneo ya kimkakati kwa maendeleo ya nchi zote mbili.