Rais Mstaafu Jakaya Dkt. Mrisho Kikwete, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia Masuala ya Elimu Duniani (Global Partnership for Education – GPE), ameendelea kuwa kinara katika kuhamasisha jitihada za upatikanaji wa fedha za kugharamia elimu kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu duniani.
Kwa nafasi yake ya Mwenyekiti wa Bodi ya GPE, Dkt. Kikwete ameongoza Mkutano muhimu wa Bodi hiyo uliofanyika Paris, Ufaransa tarehe 3–4 Juni 2026, ambao pamoja na mambo mengine umejadili mkakati wa GPE wa kukusanya Dola za Marekani bilioni 15 ifikapo mwaka 2030 kupitia kampeni ijulikanayo kama GPE 2030.
Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Bi. Éléonore Caroit, Waziri wa Nchi wa Ufaransa anayeshughulikia masuala ya Ubia wa Kimataifa na Maslahi ya Wafaransa waishio Ng’ambo.
Kupitia ubia na ushirikiano kati ya GPE, nchi wafadhili na mashirika ya kimataifa ya misaada, taasisi hiyo imelenga kuwafikia watoto takriban milioni 270 ambao kwa sasa hawapo shuleni duniani kote kutokana na sababu mbalimbali. Aidha, fedha zinazokusanywa na GPE hutumika kuboresha elimu ya awali na msingi katika nchi za kipato cha chini na zinazoendelea, hususan kwa watoto wa kike na wale wanaoishi katika mazingira magumu kama vile maeneo yaliyoathiriwa na vita, ukame na mafuriko.
Kupitia Kampeni ya GPE 2030, jumla ya wanafunzi milioni 750 kutoka nchi 96 duniani wanatarajiwa kunufaika kupitia uimarishaji wa mifumo ya elimu, upatikanaji wa vitabu vya kiada na ziada, ujenzi na ukarabati wa madarasa na maabara, pamoja na mafunzo ya kuwaongezea walimu ujuzi na uwezo wa kufundisha.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na GPE baada ya mkutano huo, nchi za Italia na Nigeria zitaongoza kampeni ya uchangishaji wa fedha hizo katika hafla maalumu itakayofanyika tarehe 23 Septemba 2026 pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UNGA).
Vilevile, taarifa hiyo imeeleza kuwa licha ya mabadiliko ya hali ya kifedha duniani, ambapo baadhi ya wafadhili hususan nchi zilizoendelea wanabadilisha vipaumbele vyao vya ufadhili, GPE imeridhishwa na mwitikio chanya kutoka kwa nchi wafadhili kama Ujerumani, Australia na Ufaransa ambazo tayari zimetangaza michango yao kwa kampeni hiyo.
Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Saidi Othman Yakubu, alihudhuria hafla iliyoandaliwa baada ya mkutano huo. Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazonufaika na fedha zinazotolewa na GPE, ambapo hadi sasa imepokea zaidi ya Dola za Marekani milioni 207.3 kwa ajili ya kuboresha sekta ya elimu nchini. Aidha, GPE imetenga takriban Dola za Marekani milioni 50 kwa ajili ya Tanzania kama sehemu ya mwendelezo wa juhudi za kuimarisha sekta hiyo muhimu.

