Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akizungumza wakati wa akizindua rasmi Bodi mpya ya Wakurugenzi ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) jijini Arusha tarehe 3 Juni 2026 ,

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akikata utepe na kumkabidhi nyenzo za kufanyia kazi Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) wakati wa uzinduzi wa Bodi mpya ya Wakurugenzi ya Shirika hilo jijini Arusha tarehe 3 Juni 2026. Kulia ni Mkurugenzi wa NHC Bw. Hamad Abdallah.

Sehemu ya wajumbe wa Bodi mpya ya Wakurugenzi ya Shirika la Nyumba la Taifa ( NHC) wakiwa katika uzinduzi wa Bodi hiyo jijini Arusha tarehe 3 Juni 2026. Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo (katikati), Mwenyekiti wa Bodi ya NHC Dk. Sophia Kongela (kushoto) na Mkurugenzi wa NHC Bw. Hamad Abdallah wakiwa katika uzinduzi wa Bodi mpya ya Wakurugenzi ya NHC jijini Arusha tarehe 3 Juni 2026.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo (Katikati waliokaa) akiwa katika picha ya Pamoja na wajumbe Bodi mpya ya Wakurugenzi ya NHC jijini Arusha tarehe 3 Juni 2026.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Leonard Akwilapo akimkabidhi nyenzo ya kufanyia kazi aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi Bi. Dorothy Mwanyika ambaye ni mjumbe wa bodi ya NHC wakati akizindua rasmi Bodi mpya ya Wakurugenzi ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) jijini Arusha tarehe 3 Juni 2026 ,(PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

……….. 

Na Mwandishi Wetu, ARUSHA

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Leonard Akwilapo, ameielekeza Bodi mpya ya Wakurugenzi ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kusimamia kwa ukaribu ukusanyaji wa mapato na madeni ya Shirika, akisisitiza kuwa hakuna mdaiwa anayepaswa kupewa upendeleo katika kulipa fedha zinazodaiwa na taasisi hiyo. 

Akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa Bodi mpya ya Wakurugenzi ya NHC uliofanyika jijini Arusha tarehe 3 Juni 2026 , Dk. Akwilapo alisema mafanikio ambayo Shirika limeyafikia katika kujiendesha kibiashara na kuendelea kuwa imara kifedha yanapaswa kulindwa kwa kuimarisha nidhamu ya mapato na usimamizi wa rasilimali zake.

“Msitishike linapokuja suala la kudai malipo yenu halali. Hakuna mdaiwa anayepaswa kuogopwa. Wote wapeni ankara zao za madeni kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo,” alisema Dk. Akwilapo.

Waziri huyo wa Ardhi alisema NHC ni miongoni mwa mashirika ya umma yaliyoendelea kuonesha uimara katika biashara zake, tofauti na baadhi ya taasisi ambazo zilishindwa kujiendesha kwa ufanisi na hatimaye kupoteza nafasi yake katika uchumi wa taifa. 

Alieleza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ina matarajio makubwa kwa NHC katika kuendeleza agenda ya makazi bora, miji endelevu na uwekezaji wa kimkakati unaochochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Dk. Akwilapo pia aliitaka Bodi mpya kusimamia kwa karibu maandalizi ya Mpango Mkakati mpya wa Shirika utakaokwenda sambamba na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mpango wa Tatu wa Taifa wa Maendeleo pamoja na malengo ya kimataifa ya maendeleo endelevu yanayohusiana na makazi na maendeleo ya miji.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah, alisema Shirika limeendelea kuimarisha utendaji wake kupitia uwekezaji katika miradi ya makazi, biashara na matumizi ya mifumo ya kidijitali inayorahisisha utoaji wa huduma na usimamizi wa shughuli zake.

Alisema NHC imeendelea kuimarisha vyanzo vya mapato kupitia upangishaji wa majengo, mauzo ya nyumba na viwanja pamoja na miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo tofauti nchini.

Bw. Hamad alibainisha kuwa Menejimenti ya Shirika itaendelea kushirikiana kwa karibu na Bodi mpya ili kuhakikisha maelekezo ya Serikali yanatekelezwa kwa ufanisi na NHC inaendelea kuwa taasisi ya mfano katika sekta ya makazi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya NHC, Dk. Sophia Kongela, alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiamini Bodi hiyo na kuwapa wajumbe dhamana ya kuiongoza taasisi hiyo katika kipindi kingine cha utekelezaji wa majukumu yake. 

Dk. Kongela alisema Bodi imepokea kwa uzito maelekezo yaliyotolewa na Waziri na iko tayari kuyafanyia kazi kwa kushirikiana na Menejimenti ya Shirika.

Alisema moja ya vipaumbele vya Bodi ni kuimarisha usimamizi wa mali za Shirika, kuongeza tija ya uwekezaji, kuimarisha ukusanyaji wa mapato, kusimamia miradi ya makazi nafuu na kuhakikisha NHC inaendelea kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya makazi nchini.

“Tunatoa hakikisho la ushirikiano wa karibu na Serikali pamoja na Menejimenti ya Shirika ili kuhakikisha NHC inafikia malengo yake na kuendelea kuwa chachu ya maendeleo ya sekta ya makazi Tanzania,” alisema Dk. Kongela.

Uzinduzi wa Bodi mpya ya Wakurugenzi ya NHC umeashiria mwanzo wa awamu mpya ya uongozi unaotarajiwa kuimarisha zaidi ukuaji wa Shirika, kuongeza uwekezaji na kuharakisha utekelezaji wa miradi ya makazi bora kwa manufaa ya Watanzania.

Bodi hiyo mpya inaongozwa na Mwenyekiti, Dk. Sophia Kongela na wajumbe wake wakiwa ni Eliud Sanga, Profesa Wilbard Kombe, Ali Hussein Laay, Doroth Mwanyika, Ayoub Omari Kasui, Vupe Ligate na Elias Kisamo.