Tanga, Juni 03, 2026

Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ), leo (Jumatano, Juni 3, 2026), zimeingia katika makubaliano rasmi ya ushirikiano kupitia mpango wa “Cash Waqf” unaolenga kuongeza upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya kufadhili elimu ya juu nchini.

Hafla hiyo imefanyika jijini Tanga ambapo mgeni rasmi alikuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma (Mb), na imeambatana na uzinduzi rasmi wa tawi la PBZ IKHLAS katika Jiji la Tanga.

Katika hotuba yake, Mhe. Mwijuma amesisitiza umuhimu wa taasisi za kifedha kuendelea kuikumbuka jamii kwa kutekeleza mipango inayochangia maendeleo ya wananchi. Ameipongeza PBZ kwa kuendelea kupanua huduma zake katika maeneo mbalimbali nchini, hatua inayoongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wananchi wengi zaidi.

Aidha, Mhe. Mwijuma amewahimiza wananchi wa Mkoa wa Tanga kutumia fursa zinazotolewa na PBZ, ikiwemo huduma za akaunti, uwekezaji na mikopo, ili kuimarisha shughuli zao za kiuchumi na kuboresha maisha yao.

Naye Mkurugenzi Mwendeshaji wa PBZ, CPA Fahad Sudi Hamid, amesema benki hiyo ilianzishwa Juni 30, 1966 kwa lengo la kutoa huduma za kifedha kwa wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla. Mwaka huu (2026) PBZ inatimiza miaka 60 tangu kuanzishwa kwake, huku ikiendelea kupanua wigo wa huduma zake katika maeneo mbalimbali nchini.

“PBZ tupo Tanzania visiwani na bara. Kwa Tanzania bara, kwa sasa tupo katika mikoa minane na tunaendelea kusogeza huduma zetu kwenye mikoa mingine nchini,” amesema CPA Fahad.

Amefafanua kuwa PBZ inatoa huduma mbalimbali za kifedha zinazokidhi mahitaji ya makundi tofauti ya wananchi, zikiwemo akaunti za wafanyabiashara, akaunti za uwekezaji, akaunti zisizo za riba pamoja na fursa mbalimbali za mikopo.

“Tuna akaunti za wafanyabiashara, akaunti za uwekezaji, akaunti zisizo za riba na fursa za mikopo. Nawasihi Watanzania kufika katika benki ili kupata huduma hizi muhimu,” amesisitiza CPA Fahad.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, amesema HESLB imeingia katika makubaliano na PBZ kwa lengo la kupanua vyanzo vya rasilimali fedha na kuwawezesha vijana wengi zaidi kupata fursa za ufadhili wa masomo.

Dkt. Kiwia amesema ushirikiano huo utaongeza uwezo wa HESLB kuwafikia wahitaji wengi zaidi, hususan wanaojiunga na mafunzo ya amali kupitia vyuo vya kati, ambao baada ya kuhitimu watapata fursa za kuajiriwa katika viwanda na sekta nyingine za uzalishaji.

Ameongeza kuwa ushirikiano huo una umuhimu mkubwa kutokana na nafasi ya PBZ katika kuhudumia wafanyabiashara na wamiliki wa viwanda kwa kuwapatia huduma mbalimbali za kifedha zinazowawezesha kuendesha shughuli zao kwa ufanisi.

Naye Meneja wa Uzingatiaji wa Shariah (Shariah Compliance Manager) wa PBZ IKHLAS, Dkt. Issa Salim Mohamed akizungumza mara baada ya utiaji saini wa makubaliano hayo, amesema mpango wa “Cash Waqf” unatoa fursa kwa watu binafsi, taasisi, wahisani na wawekezaji kuchangia au kuwekeza fedha taslimu zitakazosaidia vijana wa Kitanzania kupata elimu ya juu. Ameeleza kuwa fedha zitakazopatikana zitawasilishwa HESLB ili kuongeza fursa ya upatikanaji wa ufadhili wa elimu ya juu, huku akiwahimiza wadau mbalimbali kutumia fursa hiyo kusaidia vijana wengi zaidi kutimiza ndoto zao za kusoma elimu ya juu.

Kupitia makubaliano haya, HESLB na PBZ zinakusudia kuweka mfumo imara na endelevu wa ukusanyaji na uwekezaji wa fedha kupitia mpango wa “Cash Waqf”, kwa lengo la kuongeza wigo wa ufadhili wa elimu ya juu kwa wanafunzi wengi zaidi nchini.

Ushirikiano huu unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa fedha za mikopo ya elimu ya juu, kuimarisha uendelevu wa mfuko wa mikopo na kutoa fursa kwa idadi kubwa zaidi ya wanafunzi kufikia ndoto zao za elimu na maendeleo ya kiuchumi kwa taifa.