Na Prisca Libaga RS Arusha
Lengo ni kuendelezwa kabla ya michuano ya AFCON- 2027
RC Makalla aomba kuongezewa Wataalamu wa ardhi Mkoani Arusha
Waziri Akwilapo amshukuru Rc Makalla kwa utatuzi wa migogoro ya ardhi Mkoani Arusha
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. CPA Amos Gabriel Makalla leo Jumatano Juni 03, 2026 Ofisini kwake Jijini Arusha, amekutana na kuzungumza na Waziri wa ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Leonard Akwilapo, Mhe. Makalla akiiomba Wizara kuongeza msukumo kwa wananchi ili kuendeleza viwanja vyao walivyonunua pembezoni mwa mradi wa ujenzi wa uwanja wa michezo Jijini Arusha unaojengwa ili kutumika kwenye michuano ya AFCON- 2027.
“Viwanja vingi vimechukuliwa kule AFCON lakini wengi wameshindwa kuviendeleza, ninaomba msukumo wako Mhe. Waziri kwani sasa ipo presha baada ya kuonekana uwanja unakaribia kukamilika watu wanavitamani lakini waliochukua viwanja awali wamekaa tu bila ya kuviendeleza.” Amesema Mhe. Makalla
Akizungumzia suala hilo, Waziri Dkt. Akwilapo amesema tayari Wizara imeanza kuvichukua viwanja ambavyo wamiliki wake wameshindwa kuviendeleza, akisisitiza kuwa viwanja vile kulingana na maelekezo ya serikali si kwaajili ya kuwekeza ama kuweka akiba kwaajili ya kufanya biashara baadae, msisitizo ukiwa ni viwanja hivyo kuendelezwa mapema kabla ya michuano ya AFCON inayotarajiwa kuchezwa mwaka 2027.
Mhe. Makalla katika hatua nyingine amemueleza Waziri Akwilapo pia kuhusu upungufu wa wataalamu wa ardhi katika Mkoa wa Arusha, Waziri huyo akimueleza  kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tayari ametoa kibali cha kuajiri watumishi wapya na kumuahidi kuwa baadhi ya watumishi watakaoajiriwa watapangiwa vituo vyao vya kazi Mkoani Arusha ili kukabiliana na upungufu uliopo.
Waziri Akwilapo amemshukuru pia Mhe. Makalla kwa usimamizi wake wa karibu katika sekta ya ardhi Mkoa wa Arusha, suala ambalo limekuwa na mchango mkubwa katika mapambano dhidi ya migogoro ya ardhi, Mhe. Makalla pia akimshukuru Waziri Akwilapo kwa usaidizi wa Wizara yake katika utatuzi wa migogoro mikubwa ya ardhi iliyopo katika Mkoa wa Arusha.