Dar es Salaam. Benki ya NMB imetumia uzinduzi wa Tamasha la Twenzetu kwa Yesu kuwafikia vijana kwa ujumbe wa maadili, nidhamu ya fedha na matumizi sahihi ya huduma za kidijitali, katika jukwaa linalounganisha muziki wa injili, imani na mshikamano wa kijamii.

Akizungumza katika tamasha hilo, Meneja Mwandamizi Wateja Binafsi Benki ya NMB, Zuberi Bani, alisema ushiriki wa benki hiyo unalenga kuwa karibu na vijana na jamii kwa kuwapatia maarifa ya kifedha yanayoweza kuwasaidia kujenga tabia ya kuweka akiba, kupanga matumizi na kutumia huduma rasmi za kifedha kwa usalama. “Twenzetu kwa Yesu ni zaidi ya tamasha la muziki; ni nafasi ya kukutana na vijana, kuzungumza nao kuhusu maadili, nidhamu ya fedha na huduma zinazoweza kuwawezesha katika maisha yao ya kila siku,” alisema Bani.

Alisema NMB inaendelea kutoa suluhisho zinazogusa mahitaji ya vijana na familia, zikiwemo NMB Mtoto Account, Chipukizi na Mwanachuo, pamoja na huduma za kidijitali kama NMB Mkononi, Mshiko Fasta na NMB Pesa, zinazorahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha na kukuza utamaduni wa kuweka akiba. 

Aidha, alisema huduma ya Kikundi Account sasa inapatikana kupitia App ya NMB Mkononi, hivyo kuondoa ulazima wa mteja kufika tawini. Kupitia Twenzetu kwa Yesu, NMB imesema itaendelea kushirikiana na wadau wa kijamii katika kukuza elimu ya fedha, huduma bunifu na mshikamano unaochangia maendeleo ya vijana na jamii kwa ujumla.