Kilosa, Morogoro
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) chini ya mradi wa RISE kupitia programu ya uondoaji vikwazo katika barabara (bottleneck) umekamilisha matengenezo katika maeneo korofi ya barabara ya Ludewa-Lumbiji yenye urefu wa Kilomita 21 katika kata ya Lumbiji wilayani Kilosa mkoani Morogoro.
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua miradi ya RISE inayotekelezwa wilayani humo, Meneja wa TARURA wilaya ya Kilosa Mhandisi Juliana Masalo amesema, ukarabati huo umegharimu shilingi milioni 741 na umebadili kwa kiasi kikubwa hali ya usafiri na usafirishaji katika eneo hilo.
Amesema kazi zilizotekelezwa ni pamoja na kuchonga barabara urefu wa kilomita 21, kujenga kipande cha mita 500 kwa kiwango cha zege katika eneo lenye milima la Kinyenye pamoja na ujenzi wa mifereji ya maji yenye urefu wa mita 500.
Aidha, amesema mradi huo umehusisha ujenzi wa madaraja matano ambapo manne ni madogo na moja kubwa sambamba na kupandisha tuta na kuweka changarawe katika eneo korofi la Mgambo ambalo hapo awali lilikuwa halipitiki kabisa wakati wa mvua.
”Huku milimani wananchi wanalima mahindi, maharage na tangawizi kwa wingi lakini zamani wakati wa mvua walikuwa wanapata shida kubwa kuyafikisha mazao yao sokoni kutokana na ubovu wa barabara kwa sasa hali imebadilika”, amesema Mhandisi Masalo.
Ameongeza kuwa kupitia mradi huo imekuwa ni mkombozi kwa wananchi kwani sasa zile sehemu ambazo zilikuwa korofi kupitia mradi RISE wameweza kuzikarabati.
Kwa upande wake, Diwani wa kata ya Lumbiji Mhe. Gerald Benedict Mahungo amesema mradi huo ni ukombozi mkubwa kwa wananchi wa kata hiyo ambao kwa muda mrefu waliteseka kutokana na ubovu wa miundombinu.
”Barabara ilikuwa changamoto kubwa hasa kipindi cha mvua kwani usafirishaji wa mazao ulikuwa mgumu na hata wagonjwa na wajawazito waliopata rufaa kwenda hospitali ya wilaya walikuwa wanapata changamoto kubwa”, amesema.
Naye, Mwenyekiti wa kijiji cha Kisongwe Bw. Festo Sekaila amesema kabla ya ukarabati wa barabara bei ya mazao ilikuwa chini akitolea mfano Kg 120 za maharage zilisafirishwa kati ya shilingi 20,000-30,000 lakini kwa sasa zinasafirishwa kati ya shilingi 12,000-15000 huku bei ya mazao zikiwa zipo juu.
