Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege la Air Tanzania Company Limited (ATCL) Mhandisi Peter Ulanga, amesema shirika hilo linajiandaa kurudi rasmi kwenye safari za Dubai kuanzia katikati ya mwezi Juni hadi Agosti 2026.

Akizungumza katika mahojiano ya hivi karibuni kwenye kipindi cha Power Breakfast cha Clouds FM na Clouds Media, mahojiano ambayo pia yalirushwa na Clouds TV, Mhandisi Ulanga amebainisha kuwa safari hizo zilikuwa zimesimamishwa kwa muda kutokana na changamoto za kiusalama na machafuko ya Mashariki ya Kati.

Katika hatua nyingine ya kukuza shirika, Mkurugenzi huyo amesema kuwa Serikali ya Tanzania ina mpango wa kuinunulia ATCL ndege Tisa (09) katika kipindi cha miaka minne hadi mitano ijayo. 

Sambamba na hilo, kupitia uwekezaji na mapato ya shirika lenyewe, ATCL imejipanga kununua ndege nyingine zisizopungua arobaini (40).

Mpango huo ni sehemu ya mkakati wa kuongeza uwezo wa shirika na kupanua mtandao wake wa safari ndani na nje ya nchi.

Mhandisi Ulanga ameeleza pia kuwa ATCL imeomba vibali vya kuanza kuruka kwenda maeneo mapya ya Afrika Magharibi hasa Abidjan nchini Ivory Coast na Dakar nchini Senegal.

Lengo la upanuzi huo ni kueneza huduma za shirika na wakati huo huo kusambaza utamaduni wa Kiswahili katika mataifa yanayozungumza Kifaransa.

Akigusia utendaji wa sasa, MD huyo amesema huduma za ATCL zimeimarika kwa kiasi kikubwa kiasi kwamba zaidi ya nusu ya abiria wanaotumia ndege za Air Tanzania kwenda maeneo kama Mumbai nchini India na Guangzhou nchini China si raia wa Tanzania.

Abiria wengi wageni wanatumia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere kama kitovu cha mapito, jambo linaloonesha Dar es Salaam inazidi kujipatia hadhi ya kituo muhimu cha usafirishaji angani barani Afrika.

Katika kuhamasisha utalii na michezo ndani ya nchi, Mhandisi Ulanga ametoa mfano wa mkakati wa kuunganisha mikoa ambapo mashabiki au watalii wataweza kuangalia mchezo mkoani Arusha na baadaye kusafiri kwenda kulala Zanzibar kwa urahisi siku hiyo.

Pia amezungumzia ufunguzi wa safari mpya kuelekea Sumbawanga mkoani Rukwa kama njia ya kuchochea shughuli za kiuchumi katika mkoa huo.

Mahojiano hayo yanajiri wakati ATCL ikiendelea kupanua safari zake Afrika na nje ya Afrika chini ya uongozi wa Mhandisi Peter Ulanga ambaye aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo mwezi Novemba 2024.