Na Oscra Tarimo WMJJWM- Dodoma
Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum imeendelea kuimarisha juhudi za kulinda watoto na kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa kutekeleza afua mbalimbali katika jamii na taasisi za elimu nchini.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima ameyasema hayo tarehe 01 Juni, 2026 wakati akiwasilisja Hotuba ya utekelezaji wa Mpango wa Bajeti kwa mwaka 2025/26 na makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwakaa 2026/27 Bungeni jijini Dodoma.
Dkt. Gwajima amesema hatua hizo zimechukuliwa ili kuhakikisha watoto wanapata mazingira salama ya kukua na kuendeleza ustawi wao kwa manufaa ya Taifa.
Amesema katika kipindi cha Julai 2025 hadi Aprili 2026, jumla ya watoto 6,182 waliokuwa wanaishi na kufanya kazi mitaani waliokolewa, huku watoto 5,663 kati yao wakiunganishwa na familia zao ili kuendelea kupata malezi ya kifamilia.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, Serikali pia imetoa mafunzo kwa wawezeshaji 516 kuhusu usalama wa watoto mtandaoni, ambao baadaye waliwafikia zaidi ya wanafunzi milioni 1.8 pamoja na walimu na watumishi wa shule katika mikoa yote 26 ya Tanzania Bara.
Amesema Serikali imezindua Mkakati wa Taifa wa Kisekta wa Kutokomeza Ukeketaji wa mwaka 2025/26 hadi 2029/30 wenye lengo la kupunguza kiwango cha ukeketaji kutoka asilimia 8 hadi asilimia 4 ifikapo mwaka 2030.
Katika kuimarisha malezi bora, Wizara imeendelea kutoa elimu kwa wazazi na walezi ambapo zaidi ya watu 469,000 wamefikiwa kupitia majukwaa mbalimbali ya jamii, viongozi wa dini na wahamasishaji wa maendeleo.
Dkt. Gwajima amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha vitendo vya ukatili dhidi ya watoto na wanawake vinatokomezwa, huku ikiimarisha mifumo ya ulinzi, malezi na ustawi wa jamii kwa maendeleo ya kizazi cha sasa na kijacho.
