Na Happy Lazaro, Arusha .
Wananchi mkoani Arusha wametakiwa kujitokeza kwa wingi katika mikutano ya hadhara itakayofanyika wakati wa ziara ya Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) anayeshughulikia Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Laban Kihongosi, ambayo inalenga kuwasilisha kero, changamoto na maoni yao kwa viongozi wa chama na serikali.
Katibu wa Itikadi, Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Saipulani Ramsey, ameyasema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya ziara ya siku tatu ya Kihongosi inayotarajiwa kuanza Juni 4 hadi 6 mwaka huu.
Ramsey amesema ziara hiyo inalenga kuwasogezea wananchi viongozi wa chama na serikali ili kusikiliza changamoto zao na kutafuta ufumbuzi wa masuala mbalimbali yanayowagusa katika maisha ya kila siku.
Amesema pamoja na kusikiliza kero za wananchi, Kihongosi na ujumbe wake watapata fursa ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, maji na miundombinu.
“Wananchi watapata nafasi ya kutoa maoni kuhusu mafanikio yaliyopatikana na maeneo yanayohitaji maboresho ili kuongeza ufanisi wa huduma zinazotolewa na serikali.”amesema Ramsey.
Aidha, sehemu ya ziara hiyo itahusisha kukagua uhai wa chama katika ngazi mbalimbali kuanzia matawi, kata, wilaya hadi mkoa kwa lengo la kuimarisha CCM na kuongeza ushiriki wa wanachama katika shughuli za kisiasa na maendeleo.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa, Kihongosi ataanza ziara yake Wilaya ya Karatu Juni 4, kabla ya kuendelea Wilaya ya Arumeru Juni 5 na kuhitimisha ziara hiyo kwa mkutano mkubwa wa hadhara katika Jiji la Arusha Juni 6.
Aidha amesema kuwa,CCM Mkoa wa Arusha imesema imefanikiwa kufika katika kata 107 kati ya kata 161 zilizopo mkoani humo kupitia ziara ya awamu ya pili ya kuimarisha chama inayoongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Thomas Ole Sabaya.
Ramsey amesema ziara hizo zimekuwa daraja muhimu la kuunganisha wananchi na viongozi wa chama kwa kuwa zimewezesha wananchi kueleza changamoto zao moja kwa moja huku chama kikijipatia mrejesho wa maendeleo na huduma zinazotolewa katika maeneo mbalimbali.
“Napenda niwahakikishie CCM itaendelea kuwafuata wananchi walipo, kusikiliza maoni yao na kushirikiana na serikali kutatua changamoto zinazowakabili kwa lengo la kuharakisha maendeleo ya Mkoa wa Arusha na Taifa kwa ujumla.”amesema Ramsey.

