NA DENIS MLOWE, IRINGA
WITO umetolewa kwa wajasiriamali nchini kutumia kikamilifu fursa mbalimbali zinazowekwa na Serikali ili kuongeza uzalishaji, kupanua masoko na kukuza biashara zao kwa manufaa ya uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Benjamin Sitta, wakati akifungua mafunzo maalumu ya ujasiriamali yaliyoandaliwa na Mbunge wa Iringa Mjini na kuwakutanisha zaidi ya washiriki 400 kutoka maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Iringa
Akizungumza mbele ya washiriki hao, Sitta alisema Serikali imeendelea kuimarisha mazingira ya biashara kupitia mifumo mbalimbali ya uwezeshaji ikiwemo mikopo inayotolewa na halmashauri pamoja na fursa za manunuzi ya umma zinazowawezesha wananchi kushiriki katika zabuni za Serikali.
Alisema pamoja na uwepo wa fursa hizo, bado kuna haja kwa wajasiriamali wengi kuongeza uelewa kuhusu namna ya kuzitumia ili ziweze kuleta matokeo chanya katika biashara na shughuli zao za kiuchumi.
Mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini Fadhili Ngajilo ni mwendelezo wa mpango wa kuwajengea uwezo wajasiriamali wadogo na wa kati kupitia elimu ya biashara, usimamizi wa fedha, upatikanaji wa mitaji, utafutaji wa masoko na matumizi ya fursa za kiuchumi zilizopo ndani na nje ya mkoa wa Iringa.
Katibu Msaidizi wa Ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini, Hassan Rafiq, alisema idadi kubwa ya washiriki waliojitokeza inaonesha kuwa wananchi wengi wameanza kutambua nafasi ya elimu katika kukuza shughuli za ujasiriamali na kuongeza ushindani katika soko.
“Mwitikio wa wananchi katika awamu hii ya pili umekuwa mkubwa zaidi kuliko ilivyokuwa wakati wa mafunzo ya kwanza, hali inayotafsiriwa kuwa ishara ya kuongezeka kwa hamasa ya kutafuta maarifa yatakayowasaidia kuboresha biashara zao.” Alisema
Alisema ofisi hiyo itaendelea kuandaa mafunzo ya aina hiyo kwa nyakati tofauti ili kuwafikia wajasiriamali wengi zaidi na kuwasaidia kupata mbinu bora za kukabiliana na changamoto zinazojitokeza katika mazingira ya biashara.
Baadhi ya washiriki walioshiriki mafunzo hayo walieleza kufurahishwa na mada zilizowasilishwa, wakisema zimewapa maarifa mapya kuhusu usimamizi wa biashara, uongezaji wa faida, upatikanaji wa masoko pamoja na matumizi sahihi ya mikopo inayotolewa na taasisi mbalimbali za kifedha.
Washiriki hao walieleza matumaini yao kuwa elimu waliyoipata itawasaidia kufanya maamuzi sahihi ya kibiashara, kuongeza mtaji na kuimarisha maendeleo ya biashara zao katika kipindi kijacho.