Mei 31, 2026 saa 9:10 alasiri huko maeneo ya maji mazuri katika barabara ya Mbeya – Chunya, Gari yenye namba za usajili T134DFB aina ya Mitsubishi Basi la abiria kampuni ya Mwasote likitokea Mbeya kuelekea Chunya likiendeshwa na dereva Nehemia Sanga [50] mkazi wa Uyole iliacha njia, kupinduka na kusababisha vifo vya watu wanne wanaume 3 na mwanamke 1 umri kati ya 35 – 40.

Kati ya waliofariki wawili walitambulika ambao ni Hamza, miaka 30 na Matrida Mwabanganya, miaka kati ya 30 hadi 36. Aidha, katika ajali hiyo watu 29 walijeruhiwa kati yao wanaume 24 na wanawake 5. Majeruhi waliolazwa ni 11 na wengine 18 walitibiwa katika Hospitali ya Rufaa Kanda Mbeya na kuruhusiwa kati yao wanaume ni 17 na mwanamke 1.

Chanzo cha ajali ni uzembe wa dereva wa Gari namba T134DFB kushindwa kulimudu Gari lake katika eneo lenye kona kali kisha kuacha njia na kupinduka. Dereva huyo anaendelea kupatiwa matibabu chini ya ulinzi.

ASHIKILIWA KWA TUHUMA ZA UNYANG’ANYI WA KUTUMIA SILAHA, UVUNJAJI NA UBAKAJI.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Siwema Yona Simfukwe [24] Mfungwa aliyetoroka gerezani Mei 13, 2026 akiwa anatumikia kifungo cha miaka 30 kwa kosa la Unyang’anyi wa kutumia silaha kwa tuhuma za matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha.

Mtuhumiwa baada ya kutoroka gerezani amefanya matukio ya unyang’anyi, uvunjaji na ubakaji katika maeneo ya Iwambi, Jiji la Mbeya, miongoni mwa matukio hayo ni tukio la Mei 15, 2026 saa 2:30 usiku huko Iwambi ambapo alivamia nyumba ya mwananchi mmoja akiwa na silaha [Panga] na kutishia kumuua mtoto wa familia hiyo endapo hawatatii amri yake, kisha kuwafunga kamba na kumbaka Mama na Binti wa kazi, kupora simu mbili aina ya Iphone 15 na 16 pamoja na fedha taslim shilingi 400,000/=. 

Aidha, Mei 22, 2026 saa 3 usiku huko Iwambi alivamia nyumba ya mwananchi mwingine na kupora simu aina ya Iphone 11 Plain na fedha taslimu shilingi 300,000/= zilizokuwa kwenye simu kwa kumuamuru atoe nywila (Password) ya simu na kufanikiwa kuhamisha fedha hizo.

Kufuatia matukio hayo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya kupitia Askari maalum wa kuzuia na kupambana na matukio ya uhalifu lilifanya msako na Mei 30, 2026 saa 10:30 jioni huko Chipaka Wilaya ya Momba, Mkoa wa Songwe lilifanikiwa kumkamata mtuhumiwa Siwema Yona Simfukwe [24] kwa tuhuma za makosa hayo. 

Mtuhumiwa alikutwa na Silaha iliyotengenezwa kienyeji, Panga, Risasi ya Shot Gun moja na mizura miwili iliyokuwa ndani ya mifuko. Kitendo cha kupatikana na silaha hizo kulizua hasira kwa wananchi ambao walianza kumshambulia mtuhumiwa, hata hivyo Jitihada za Askari Polisi zilifanikiwa kumuokoa na kumkimbiza Hospitali ya Rufaa Mbeya kwa matibabu.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa madereva kuwa makini wawapo barabarani ikiwa ni pamoja na kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepuka ajali. Aidha, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea kutoa rai kwa baadhi ya wananchi kuacha uhalifu kwani hauna nafasi katika jamii na halitasita kumkamata na kumchukulia hatua za kisheria yeyote atakayebainika kujihusisha na uhalifu.