Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Mhe. Profesa Kitila Alexander Mkumbo akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu kuanza Utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 (DIRA2050), tarehe 31 Mei, 2026 Ikulu, Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) Ndugu Gilead Teri akizungumza na Waandishi wa Habari juu ya mikakati ya kuvutia uwekezaji wakati wa mkutano wa taarifa ya Tume ya Taifa ya Mipango kuanza Utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 (DIRA2050) tarehe 31 Mei, 2026 Ikulu, Dar es Salaam.
………….
Na John Bukuku, Ikulu- Dar es Salaam
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa maelekezo mbalimbali yatakayohakikisha utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unaanza kwa ufanisi kuanzia Julai 1, 2026.
Profesa Mkumbo ameyasema hayo leo Mei 31, 2026 Ikulu jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maamuzi, maagizo na maelekezo yaliyotolewa na Rais Samia katika kikao cha Tume ya Taifa ya Mipango kilichofanyika Mei 26, 2026.
Amesema katika kikao hicho kilichoongozwa na Rais Samia, Tume ya Taifa ya Mipango ilijadili na kuidhinisha miongozo minne muhimu itakayotumika kusimamia utekelezaji wa Dira 2050, ambayo ni Mwongozo wa Kitaifa wa Mipango, Mwongozo wa Kitaifa wa Uidhinishaji wa Miradi ya Maendeleo, Mwongozo wa Kitaifa wa Ufuatiliaji na Tathmini ya Miradi ya Maendeleo pamoja na Mkakati wa Mawasiliano wa Dira 2050 wa miaka mitano kuanzia mwaka 2026/27 hadi 2030/31.
Profesa Mkumbo amesema Tume pia imeidhinisha maeneo matatu makubwa ya kimkakati yatakayopimwa kupitia viashiria 142 ili kufuatilia maendeleo ya utekelezaji wa dira hiyo.
Maeneo hayo ni mageuzi katika mifumo ya utawala na utumishi wa umma yenye viashiria 13, mageuzi katika uwekezaji na uzalishaji yenye viashiria 53 na mageuzi katika maendeleo ya kijamii, kiuchumi na mazingira yenye viashiria 76.
Aidha, amesema Tume imepitisha sekta 12 za kipaumbele zilizobainishwa katika Mpango wa Nne wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2026/27–2030/31), ambazo zitafuatiliwa kupitia viashiria 206 vya upimaji.
Sekta hizo ni pamoja na kilimo, viwanda na ujenzi, madini na nishati, utalii, michezo na sanaa, sekta ya ubunifu na maudhui ya kidigitali, ardhi na maendeleo ya miji, biashara na uwekezaji, elimu, hifadhi ya jamii, kazi na ustawi wa jamii, uchumi wa buluu pamoja na sayansi, teknolojia, ubunifu na uchumi wa kidigitali.
Akizungumzia usimamizi wa utekelezaji wa mipango ya maendeleo, Profesa Mkumbo amesema Rais Samia ameelekeza Sekretarieti ya Tume ya Taifa ya Mipango kujielekeza zaidi katika kusimamia utekelezaji wa mipango badala ya kuishia katika maandalizi ya sera na mikakati.
Amesema Rais pia ameelekeza kuwa wakati Tume haijakutana chini ya uenyekiti wake, wajumbe wa Tume watafanya kazi kama Ofisi ya Usimamizi wa Utekelezaji wa Mipango (Delivery Bureau) chini ya uongozi wa Makamu Mwenyekiti wa Tume kwa lengo la kuhakikisha utekelezaji wa mipango unasimamiwa kwa karibu na kwa matokeo yanayoonekana.
Katika hatua nyingine, Profesa Mkumbo amesema Tume imeagiza kuharakishwa kwa majadiliano kati ya Serikali na wawekezaji kuhusu miradi mikubwa ya kimkakati inayotarajiwa kuwa chachu ya ukuaji wa uchumi, uwekezaji na ajira nchini.
Ametaja miradi hiyo kuwa ni mradi unganishi wa chuma cha Liganga na makaa ya mawe ya Mchuchuma, mradi wa magadi soda wa Engaruka, mradi wa kuchakata gesi asilia kuwa kimiminika (LNG) pamoja na Mradi wa Nikeli wa Kabanga na kiwanda cha usafishaji wa madini kitakachojengwa Kahama.
Profesa Mkumbo amesema utekelezaji wa miradi hiyo ni sehemu muhimu ya kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na Mpango wa Nne wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano, huku akisisitiza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha miradi hiyo inaanza kutoa matokeo yanayotarajiwa kwa maendeleo ya taifa.

