NA DENIS MLOWE,  IRINGA 
MENEJA wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoa wa Iringa, Peter Jackson, amesema kuwa tasnia ya maziwa ni eneo muhimu katika kukuza uchumi wa wananchi na taifa kwa ujumla. 
Alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari wa Full Shangwe wakati alipotembelea maonyesho ya wiki ya 29 ya maziwa yanayofanyika kitaifa katika viwanja vya Mwembetogwa, mkoani Iringa nchini Tanzania.
Jackson alisema kuwa maonyesho hayo yanatoa fursa pana ya kuongeza uelewa kwa wananchi, kujifunza teknolojia mpya na kuhamasisha uwekezaji zaidi katika sekta ya maziwa, sekta inayogusa maisha ya wakulima, wafugaji na watu wengi wanaojihusisha na biashara na uchakataji wa maziwa.
Akizungumzia umuhimu wa tasnia hiyo, alisema kuwa maziwa na bidhaa zake zimekuwa na mahitaji makubwa ndani na nje ya nchi, hali inayochochea kukua kwa uchumi wa jamii na taifa. 
Alieleza kuwa bidhaa kama maziwa mtindi, jibini, siagi na ghee zimekuwa chanzo cha ajira kwa vijana na wanawake, huku viwanda vidogo na vya kati vikiongeza thamani ya maziwa na kuchangia mapato ya serikali kupitia kodi.
Jackson alisisitiza kuwa jukumu la TRA ni kuwezesha wafanyabiashara kufuata taratibu kwa urahisi, ikiwemo usajili wa Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN), matumizi ya mashine za kielektroniki za kutolea risiti (EFD) na kulipa kodi kwa usahihi.
 Alisema kuwa lengo la TRA si kuwabana wafanyabiashara, bali kujenga mazingira rafiki na wezeshi kwao.
Akizungumzia changamoto, Jackson alitaja miundombinu duni ya uhifadhi wa maziwa, elimu ndogo kuhusu ubora wa bidhaa, na upatikanaji mdogo wa masoko ya uhakika kama baadhi ya vikwazo vinavyokabili sekta ya maziwa.
 Aliongeza kuwa kupitia ushirikiano kati ya serikali, wadau wa sekta na taasisi za kifedha, changamoto hizo zinaweza kupatiwa suluhisho la kudumu.
Katika maonyesho hayo, washiriki kutoka maeneo mbalimbali, taasisi za serikali, vyuo na kampuni binafsi walionyesha teknolojia mpya za uchakataji maziwa na mbinu bora za uzalishaji. Jackson alisema kuwa maonyesho hayo ni jukwaa muhimu la kuwakutanisha wazalishaji, watumiaji na wawekezaji, sambamba na kutoa elimu kwa vijana kuhusu fursa zilizopo katika sekta ya maziwa.
Jackson aliwataka wananchi, wafugaji na wafanyabiashara kutumia fursa zilizopo katika maonyesho hayo na kuongeza uzalishaji wa maziwa huku wakizingatia ulipaji sahihi wa kodi ili kuiwezesha serikali kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo.