Na.Sophia Kingimali
Katika hatua ya kuhamasisha uandishi wa habari unaogusa maisha ya wananchi moja kwa moja, Shirika la MSI Tanzania limezindua rasmi Tuzo ya Uandishi wa Habari za Afya ya Uzazi ndani ya Tuzo za Umahiri wa Uandishi wa Habari Tanzania (EJAT) 2025.
Tuzo hiyo mpya inalenga kuongeza hamasa kwa wanahabari kuandika taarifa zenye kuelimisha jamii kuhusu afya ya uzazi, huku ikitambua mchango wa vyombo vya habari katika kuleta mabadiliko ya kijamii na kiafya nchini.
Akizungumza leo Mei 28, 2026 jijini Dar es salaam wakati Baraza la Habari Tanzania (MCT) likitangaza majina ya wateule wa EJAT 2025, Katibu Mtendaji wa MCT, Ernest Sungura, amesema maboresho ya tuzo hizo yanalenga kuendana na mabadiliko ya sekta ya habari na kuongeza nafasi kwa taaluma maalumu za uandishi.
Mbali na tuzo ya afya ya uzazi, makundi mengine mapya yaliyoingizwa mwaka huu ni pamoja na Tuzo ya Mahojiano Bora ya Mwaka, Tuzo ya Kijana Chipukizi, Tuzo ya Uandishi wa Habari za Elimu ya Uwezo Tanzania pamoja na Tuzo ya Uhifadhi ya Mwalimu Julius Nyerere.
Wateule waliotajwa kuwania EJAT 2025 ni pamoja na Julius Maricha wa The Citizen, Halima Mlacha wa Habari Leo, Hamadi Rashid wa The Loyal Media na UN Radio, Leonard Mubale wa TriGen Media, Philip Mwihava wa Clouds FM na Manyerere Jackton wa Jamhuri Media.
Kwa upande wa taasisi za habari, Azam Media, Nukta Africa, Mwananchi Newspaper, The Guardian Newspaper, Tanzania Standard Newspapers (TSN) na Jamhuri Newspaper zimefanikiwa kuingia hatua ya mwisho ya tuzo hizo.
Mkurugenzi Mkazi wa MSI Tanzania, Patrick Kinemo, amesema taasisi hiyo imeendelea kushirikiana na Wizara ya Afya tangu mwaka 1989 katika kuboresha huduma za afya ya uzazi na uzazi wa mpango, hasa kwa wananchi wa maeneo yenye changamoto ya upatikanaji wa huduma.
Amesema MSI inaamini vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kusambaza taarifa sahihi za afya ya uzazi na kusaidia jamii kufanya maamuzi sahihi kuhusu afya zao.
Kwa mujibu wa Kinemo, ndani ya miaka minne ya ushirikiano kati ya MSI na MCT, wanahabari zaidi ya 30 wamepata mafunzo maalumu huku zaidi ya habari 100 kuhusu afya ya uzazi zikirushwa na kuchapishwa, hatua iliyosaidia kuongeza uelewa wa wananchi pamoja na kuwafikia watunga sera.
Washindi wa EJAT 2025 wanatarajiwa kutangazwa Mei 29 katika hafla maalumu itakayofanyika Hoteli ya Four Points by Sheraton jijini Dar es Salaam.

