Na Mwandishi Maalum,Mbinga
BAADHI ya wakulima wa zao la kahawa wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma,wamewaomba wawekezaji na wadau kujitokeza kufunga mitambo ya kisasa ya kuchakata zao hilo ili kuhamasisha jamiii unywaji wa kahawa wanayolima na kuongeza thamani ya soko la kahawa.
Mkulima wa zao la kahawa Ami Kayuza amesema,kukosekana kwa mitambo ya kisasa ya kuchakata zao hilo kumesababisha baadhi ya wakulima kupeleka kahawa nje ya wilaya ya Mbinga kufuata huduma uchakataji ili waweze kupata kahawa bora itakayokubalika kwenye soko la ndani na nje ya mkoa wa Ruvuma.
Aidha Kayuza,ameishukuru kampuni ya Hagati Company Ltd kuwajengea kiwanda cha kisasa cha kuchakata kahawa ambacho kinalenga kuimarisha soko la kahawa na kuondoa changamoto iliyokuwa ikiwakabili ya kusafirisha kahawa wanayozalisha kwa muda mrefu.
Kayuza alisema,kiwanda hicho kimewawezesha wakulima kuanza kuuza kahawa iliyosindikwa kwenye masoko ya ndani na nje ya wilaya ya Mbinga na kuhamasisha unywaji wa kahawa kwa watu mbalimbali ndani na nje ya wilaya ya Mbinga.
“kiwanda cha Hagati kitarahisisha huduma za wakulima na kuwapunguzia mzito wa kusafirisha kahawa za maganda kupeleka makambako au mkoani Mbeya,tunapongeza sana kuanzishwa kwa kiwanda hiki kwa sababu Mbinga uzalishaji wa kahawa ni mkubwa kuliko wilaya nyingine za mkoa wa Ruvuma”alisema Kayuza.
Mkulima wa kijiji cha Kipapa Astel Hili,ameipongeza kampuni hiyo kwa kuanzisha kiwanda hicho ambacho kitasaidia kuongeza thamani na kuuza kahawa iliyosindikwa badala ya kuuza kahawa ghafi ambayo faida yake ni ndogo ikilinganisha na iliyosindikwa.
“Naipongeza sana kampuni ya Hagati kutuletea kiwanda hiki cha kisasa,kiukweli kwa sasa tunafanya biashara yetu ya kahawa iliyosindikwa na tunapata wateja wengi wakubwa na wadogo wanaotoka maeneo mbalimbali ya wilaya ya Mbinga na mkoa wa Ruvuma”alisema.
Mkulima mwingine Alushani Mhagama alisema,ujio wa kiwanda cha Hagati coffee kimewasaidia kuhamasisha wananchi wengi zaidi kulima kahawa katika msimu wa kilimo 2025/2026 kwani kipo karibu na maeneo yao ya uzalishaji.
Aidha,amewataka wananchi kuwa na mazoea ya kunywa kahawa kwa ajili ya kuboresha afya kwa kuwa hivi sasa kahawa imeboreshwa zaidi kutoka kutwanga kwenye kinu hadi kuchakatwa kwa kutumia mashine za kisasa.
Mmoja wa wadau wa zao la kahawa Abubakari Hagati alisema,ameamua kuanzisha kiwanda cha kuchakata kahawa ili kuwasaidia wakulima kwa kuanzisha kiwanda cha kuchakata zao hilo ili kuliongezea mnyororo wa thamani na soko kwa ujumla.
Alisema,kiwanda hicho cha kisasa kitawasaidia wakulima kuchakata kahawa ghafi ambayo itaongeza thamani kubwa na wakulima kupata fedha nyingi.
Abubakar alisema,mkakati wa Hagati Company Ltd kupitia bidhaa zake za Hagati Coffee ni kusogeza huduma bora na kuunga mkono mkakati wa Serikali wa kuhamasisha jamii kupenda kunywa kahawa yenye umuhimu mkubwa kwa afya ya binadamu.
Afisa masoko wa kampuni ya Hagati Coffee Ltd David Richard alisema,wameona ni vyema kufungua kiwanda cha kisasa kama sehemu ya kuongeza mnyororo wa thamani ya zao la kahawa na kuhamasisha wakulima wenyewe hususani wa bonde la Hagati kupenda kunywa kahawa.

