Na Albano Midelo
Baada ya kushika nafasi ya 25 kati ya mikoa 26 katika mashindano ya UMITASHUMTA mwaka uliopita, Mkoa wa Ruvuma sasa umeanza rasmi operesheni kubwa ya kurejesha heshima yake kwenye ramani ya michezo ya shule nchini Tanzania kupitia maandalizi mapya, kambi maalumu na uwekezaji wa muda mrefu katika vipaji vya vijana.
Uzinduzi wa mashindano ya kimkoa uliofanyika katika Uwanja wa Majimaji mjini Songea umebeba matumaini mapya huku viongozi wa serikali wakiahidi mageuzi yatakayoufanya mkoa huo kuwa kitovu cha michezo nchini.
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, alisema matokeo mabaya ya mwaka jana yamekuwa chachu ya kuanzisha mfumo mpya wa maandalizi ya mwaka mzima badala ya kusubiri mashindano ya UMITASHUMTA pekee.
Tunataka michezo iwe sehemu ya maisha ya wanafunzi kila siku. Ushindi unatokana na nidhamu, maandalizi na mshikamano, alisema Ahmed.
Mashindano ya taifa ya UMITASHUMTA yanatarajiwa kufanyika mkoani Iringa Juni mwaka huu huku Ruvuma ikilenga kufanya vizuri zaidi kupitia timu zilizopitia maandalizi maalumu.
Katika kuimarisha sekta hiyo, serikali imeanza kuboresha miundombinu ya michezo katika shule za Maposeni, Chandarua na Mahanje Sekondari ikiwa ni sehemu ya mkakati wa taifa wa kuibua vipaji mapema.
Kaimu Afisa Elimu Mkoa wa Ruvuma, Mathias Tilia, alisema tathmini ya kina ilibaini kuwa maandalizi hafifu, uhaba wa vifaa na muda mfupi wa kambi vilichangia matokeo mabaya ya mwaka jana.
Hata hivyo, wananchi wameeleza bado kuna changamoto za viwanja, vifaa na uelewa mdogo wa baadhi ya wazazi kuhusu umuhimu wa michezo kwa watoto wao.
