Na John Walter -Dodoma
Sekretarieti ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Manyara leo Mei 27, 2026 imemtembelea nyumbani kwake Jijini Dodoma Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Manyara ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais – Utumishi na Utawala Bora, Regina Ndege Qwaray, kwa lengo la kumpongeza kufuatia uteuzi wake uliofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ziara hiyo iliongozwa na Katibu wa CCM Mkoa wa Manyara, Shabani Mrisho, ambaye amesema uteuzi huo ni heshima kubwa kwa Mkoa wa Manyara na unaonesha imani kubwa ambayo Rais ameendelea kuwa nayo kwa viongozi wanaotoka mkoani humo.
Katibu huyo amesema Mkoa wa Manyara umebahatika kupata manaibu mawaziri wawili katika Serikali ya Awamu ya Sita, jambo ambalo linaonesha namna Rais anavyouthamini mkoa huo pamoja na viongozi wake.
Aidha amesema mbali na nafasi hizo za manaibu mawaziri, Mkoa wa Manyara pia unatoa Naibu Spika wa Bunge, Daniel Sillo, hali ambayo amesema ni ishara ya kuaminiwa kwa viongozi wa Manyara katika utendaji wa Serikali na chama.
Katika mazungumzo hayo, Katibu huyo wa CCM Mkoa wa Manyara aliwakumbusha viongozi hao kuendelea kutekeleza Ilani ya CCM kwa vitendo kwa kuwahudumia wananchi na kusimamia maendeleo ya Mkoa wa Manyara pamoja na taifa kwa ujumla.
Akizungumza baada ya kupokea ujumbe huo, Naibu Waziri Regina Ndege Qwaray aliishukuru Sekretarieti ya CCM Mkoa wa Manyara kwa kumtembelea na kumuunga mkono katika majukumu yake ya uongozi.
Amesema ataendelea kufanya kazi kwa bidii kama anavyoelekeza Rais, kwa lengo la kuwatumikia wananchi wa Mkoa wa Manyara na Watanzania wote kwa ujumla.
“ Mimi ni zao la CCM, hivyo nina wajibu mkubwa wa kutekeleza majukumu yangu kwa uaminifu na kwa nguvu zote. Imani aliyonipa Rais ni lazima niitendee haki kwa kufanya kazi kwa bidii,” amesema Regina.

