Na Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Bungeni Dodoma
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo amesema Wizara imejipanga kuanzisha Mabaraza ya Ardhi na Nyumba katika wilaya zote nchini ili kuongeza upatikanaji wa haki kwa wananchi.
Dkt. Akwilapo amesema hayo leo Mei 28, 2026 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Amesema katika mwaka 2025/2026, Wizara ilipanga kuanzisha Mabaraza mapya 24 pamoja na kushughulikia mashauri 16,000 ya ardhi.
Ameeleza kuwa hadi Mei 15, 2026, Wizara imeanzisha Mabaraza mapya sita na kufanya jumla ya Mabaraza yanayofanya kazi nchini kufikia 121.
Aidha, amesema mashauri 23,426 yamesikilizwa ambapo kati ya hayo mashauri 12,644 yamepatiwa uamuzi huku mashauri 10,782 yakiendelea kushughulikiwa.
Katika mwaka 2026/2027 Wizara itaanzisha Mabaraza mapya 18 ili kufikia lengo la kuwa na Mabaraza ya Ardhi na Nyumba katika wilaya zote 139 nchini.
Ametoa wito kwa wenyeviti wa Mabaraza hayo kuzingatia weledi, uadilifu na misingi ya utoaji haki ili kujenga imani kwa wananchi wanaopata huduma hizo.
