Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Bungeni Dodoma 

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo amesema Serikali kupitia Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) inaendelea kutekeleza mradi wa Samia Housing Scheme wa ujenzi wa nyumba 5,000 nchi nzima unaotarajiwa kugharimu shilingi bilioni 466.Dkt. Akwilapo ameyasema hayo leo Mei 28, 2026 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Amesema katika mwaka 2025/2026, Shirika la Nyumba la Taifa lilipanga kuendelea na awamu ya pili ya utekelezaji wa mradi huo kwa kujenga nyumba 908 katika maeneo mbalimbali nchini.

Ameeleza kuwa hadi Mei 15, 2026, ujenzi wa nyumba 68 za makazi katika eneo la Iyumbu mkoani Dodoma umekamilika na kufanya jumla ya nyumba zilizokamilika kufikia 628.

Aidha, amesema ujenzi wa nyumba 260 katika eneo la Mtoni Kijichi umefikia asilimia 30 huku nyumba 160 zinazojengwa Medeli, Dodoma zikifikia asilimia 25 ya utekelezaji.

Aidha, maandalizi ya ujenzi wa nyumba 100 katika maeneo ya Iyumbu na Njedengwa mkoani Dodoma pamoja na Kawe jijini Dar es Salaam yanaendelea,” amesema Dkt. Akwilapo.