Na. Meleka Kulwa-Fullshangwe Blog, Bungeni Dodoma

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Leonard Akwilapo amesema kuwa Serikali imeendelea kutekeleza maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusu utatuzi wa migogoro ya ardhi katika vijiji na mitaa 975 nchini.

Amebainisha kuwa utekelezaji wa maamuzi hayo umewezesha kurejeshwa kwa ekari milioni 3.13 za ardhi kwa wananchi waliokuwa wameathirika kutokana na migogoro mbalimbali ya matumizi ya ardhi.Dkt. Akwilapo ameyasema hayo leo Mei 28, 2026 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027.

Amesema kuwa Serikali pia imelipa fidia ya Shilingi bilioni 95.27 kwa wananchi waliostahili katika maeneo 14 yaliyohusika na utekelezaji wa mpango huo.Aidha, ameongeza kuwa Wizara imeandaa mpangokazi maalum wa kukamilisha kazi zilizobaki kwa kushirikiana na Wizara za kisekta pamoja na taasisi mbalimbali za Serikali.

Pia amebainisha kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha wananchi wanarejeshewa haki zao za ardhi na kuondoa migogoro inayochelewesha maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika maeneo mbalimbali nchini.