NA: DK. REUBENI LUMBAGALA, TANGA
Katika ulimwengu wa sasa wa ushindani wa kimaendeleo kuanzia mtu binafsi hadi ngazi ya taifa, suala la wananchi kuwa na elimu ya fedha ni muhimu sana. Hii inatokana na ukweli kuwa elimu hiyo inasaidia kuweka mipango na kufikia malengo na maendeleo ikiwa itawekwa katika utekelezaji.
Elimu ya fedha inasaidia kuwa na nidhamu ya fedha ili kufikia malengo tarajiwa na kuwa na jicho la kuona fursa mbalimbali za kuwekeza mtaji ili kuongeza kipato na kuchangia maendeleo ya nchi.
Aidha, elimu hiyo inawezesha kuwa na utamaduni wa kupanga matumizi sahihi na kuweka akiba ikiwa ni msingi wa kuwa na mtaji wa kuwekeza na kupanua biashara na uwekezaji unaofanywa na mhusika.
Wanafunzi wa vyuo ni wadau muhimu katika mipango ya uchumi na maendeleo. Wapo vyuoni wakisoma programu mbalimbali ili kuja kutumikia taifa lao na kupata maendeleo.
Kutokana na umuhimu wa elimu ya fedha katika maendeleo, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) wamekubaliana kutoa elimu ya fedha kwa wanafunzi wa vyuo.
Makubaliano hayo yamefanyika Mei 18, 2026, katika ofisi za BoT Jijini Dodoma na kuhudhuriwa wadau mbalimbali wakiongozwa na wakuu wa taasisi hizo mbili ambao ni Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk. Bill Kiwia.
Taasisi hizi zimekubaliana kuwafikia wanavyuo hasa kwa njia za kidijitali ili kuwapa elimu ya fedha. Ikumbukwe kuwa wanavyuo pia ni wanufaika wa mikopo inayotolewa na serikali kupitia HESLB na taasisi nyingine za umma na binafsi.
Hivyo basi, elimu ya fedha itawasaidia kuwa na matumizi mazuri ya fedha hizo na kuzitumia katika masuala ya msingi pekee na si starehe. Vilevile, itakuwa na jukwaa zuri kwa wanavyuo hao kuwa na matumizi mazuri ya fedha hata baada ya kumaliza masomo yao na kuingia katika ajira na kujiajiri.
Katika hafla hiyo, Gavana Tutuba alisema “Ninaipongeza HESLB kwa kutambua umuhimu wa elimu ya fedha kwa wanafunzi na kwa kushirikiana na BoT katika utekelezaji wa mpango huu muhimu. Vilevile, ninathamini juhudi zilizofanywa na timu za wataalam kutoka taasisi zote mbili katika kuandaa Hati hii ya Makubaliano”.
Taasisi hizi zina watalam wa masuala ya fedha, uchumi, biashara, uwekezaji na teknolojia ya mawasiliano, hivyo ni jukumu la wanavyuo kufanyia kazi elimu watakayoipata kwa manufaa yao hasa katika kujenga msingi wa kujiajiri, uwekezaji, biashara na maendeleo kwa ujumla wawapo vyuoni na hata baada ya kuhitimu masomo yao.
Dk. Kiwia ameonyesha matumaini makubwa juu ya elimu hiyo kwa wanavyuo katika kusaidia uwezeshaji wa wanafunzi hasa katika nyanya ya kiuchumi.
“Kupitia elimu hii ya fedha, ni matumaini yetu makubwa kuwa wanafunzi watajenga nidhamu ya fedha, kujiwekea mipango ya fedha, kuelewa umuhimu wa kuweka akiba, pamoja na kutimiza wajibu wao wa kurejesha mikopo kwa wakati. Hii utasaidia kuongeza uendelevu na ustahimilivu wa mfuko wa mikopo ya wanafunzi na kuwezesha wanafunzi wengi zaidi kunufaika miaka ijayo,” amesisitiza Dk. Kiwia.
Kwa hakika, nawapa kongole sana BoT na HESLB kwa kuja na mkakati huu mzuri wa kimaendeleo kwa wanavyuo nchini. Ni vyema wanafunzi wakazingatia mafunzo hayo yatakayotolewa kupitia mfumo wa akaunti binafsi ya wanafunzi uitwao Student’s Individual Permanent Account (SIPA).
Kimsingi, elimu ya fedha si tu ina manufaa kwa wanafunzi lakini pia kwa taifa kwani itasaidia kujenga kizazi chenye maarifa na ujuzi wa kutosha wa masuala ya fedha, uchumi, biashara na uwekezaji, jambo ambalo ni muhimu sana katika kuchagiza maendeleo ya nchi. Wanavyuo tumieni vyema fursa hiyo ya kipekee.

Maoni : 0620 800 462.
