Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiteta jambo na baadhi ya wasanii walioongozana naye nchini Korea katika moja ya ziara zake.
…………..,
Na John Bukuku, Dar es Salaam
Uamuzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuendelea kufungua milango ya uwezeshaji wa vijana kupitia mikopo ya Mfuko wa Utamaduni umeendelea kuonekana kama hatua muhimu katika kukuza uchumi wa ubunifu na ujasiriamali nchini. Kupitia mpango huo, vijana wanaojihusisha na sanaa, muziki, filamu, maigizo, ubunifu wa kidigitali pamoja na shughuli mbalimbali za biashara na ujasiriamali wanapewa nafasi ya kupata mitaji ya kukuza shughuli zao.
Katika miaka ya hivi karibuni, sekta ya sanaa, ubunifu na biashara ndogo ndogo zimekuwa chanzo kikubwa cha ajira kwa vijana wengi nchini. Wapo vijana wanaotegemea muziki, filamu, ushonaji, biashara za mtandaoni, huduma za kidigitali, upigaji picha, vipodozi, usafirishaji, kilimo biashara pamoja na shughuli nyingine za ujasiriamali kujipatia kipato cha kila siku. Hivyo, mikopo hiyo imeonekana kuwa miongoni mwa njia muhimu za kuwawezesha vijana kujikwamua kiuchumi.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Utamaduni na Sanaa Tanzania uliochini ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nyakaho Mahemba
Hata hivyo, pamoja na dhamira njema ya Serikali, bado kuna changamoto kadhaa zinazofanya vijana wengi kushindwa kunufaika kikamilifu na fursa hiyo.
Dhamana bado ni changamoto kubwa
Mojawapo ya changamoto kubwa ni suala la dhamana. Taasisi nyingi za kifedha bado zinahitaji dhamana rasmi kama nyumba, viwanja au mali nyingine zinazotambulika kisheria kabla ya kutoa mikopo.
Tatizo ni kwamba vijana wengi wanaojihusisha na sanaa, ubunifu na biashara ndogo ndogo hawana mali hizo. Wengi bado wako kwenye hatua za kujijenga kiuchumi huku mtaji wao mkubwa ukiwa ni vipaji, ubunifu au biashara wanazoziendesha kwa mtaji mdogo.
Kutokana na hali hiyo, hata kijana mwenye biashara nzuri au msanii mwenye uwezo mkubwa wa kuzalisha mapato anaweza kushindwa kupata mkopo kwa sababu hana nyumba wala kiwanja cha kuweka dhamana.
Wapo wanaoamini kuwa ipo haja ya taasisi za fedha kuanza kuangalia mbinu mbadala za dhamana, ikiwemo kutumia vikundi vya vijana, mikataba ya kazi, mapato ya kidigitali au historia ya mzunguko wa fedha kwenye akaunti za biashara kama sehemu ya vigezo vya kukopesheka.
Kutokuaminika nako ni changamoto
Pamoja na changamoto ya dhamana, suala jingine kubwa ni vijana wenyewe kutokuaminika kutokana na historia ya baadhi yao kushindwa kurejesha mikopo waliyopewa hapo awali.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyowahi kutolewa na viongozi wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), baadhi ya wasanii waliowahi kukopeshwa kupitia mifumo mbalimbali ya uwezeshaji hawakurejesha mikopo hiyo kwa mujibu wa makubaliano.
Hali hiyo imeendelea kuathiri taswira ya vijana wengi mbele ya taasisi za kifedha. Taasisi hizo zinapoona historia ya mikopo kutorejeshwa, huongeza masharti magumu au kuwa waangalifu zaidi kutoa mikopo kwa vijana wengine.
Matokeo yake ni kwamba hata vijana waaminifu wenye miradi mizuri hujikuta wakikosa nafasi kutokana na makosa yaliyofanywa na wengine waliopita.
Hivyo, ipo haja kwa vijana kuelewa kuwa mikopo si msaada wa bure, bali ni mtaji wa maendeleo unaopaswa kurejeshwa kwa wakati ili kuwapa nafasi wengine kunufaika.
Elimu ya fedha bado haijawafikia vijana wengi
Pamoja na changamoto hizo, kuna jambo jingine muhimu ambalo linaonekana kuwa mzizi wa matatizo mengi — ukosefu wa elimu ya kutosha kuhusu masuala ya fedha na mikopo.
Kwa kiasi kikubwa, elimu inayotolewa na taasisi za fedha bado haijawafikia vya kutosha vijana wengi wa sekta ya sanaa, ubunifu na ujasiriamali. Vijana wengi bado hawaelewi hata hatua za msingi zinazotakiwa kabla ya kufikiria kuomba mkopo.
Picha ikionesha studio ya kutengeneza muziki
Mfano halisi ni pale unapomuuliza kijana kama ana TIN Number ya Tanzania Revenue Authority (TRA), anakujibu kwa kuuliza “TIN Number ndiyo nini?” Hali hiyo inaonyesha bado kuna pengo kubwa la uelewa kuhusu mifumo rasmi ya biashara na fedha.
Kwa mazingira hayo, inakuwa vigumu kwa kijana kuelewa hata masharti mengine muhimu yanayotakiwa na taasisi za kifedha kama:
Kuwa na akaunti ya biashara;
Kuwa na leseni au usajili wa biashara;
Kutunza kumbukumbu za mapato;
Kuwa na mpango wa biashara;
Kuelewa mfumo wa kodi;
Na kujenga historia nzuri ya matumizi ya fedha.
Ukweli ni kwamba vijana wengi wana vipaji, mawazo mazuri ya biashara na ndoto kubwa, lakini hawajapata elimu ya kutosha kuhusu namna ya kuingia rasmi kwenye mfumo wa biashara unaotambulika na taasisi za fedha.
Taasisi za fedha zinapaswa kushuka chini zaidi
Kutokana na hali hiyo, wapo wanaoamini kuwa taasisi za fedha, mifuko ya uwezeshaji pamoja na wadau wa maendeleo wanapaswa kuongeza nguvu zaidi katika utoaji wa elimu kwa vijana.
Elimu hiyo isibaki kwenye semina za mijini pekee au matangazo ya jumla, bali iwafikie moja kwa moja vijana waliopo kwenye studio za muziki, vikundi vya sanaa, masoko, maeneo ya biashara na vituo vya ubunifu.
Vijana wanahitaji kufundishwa hatua kwa hatua kuhusu:
Namna ya kuanzisha biashara rasmi;
Umuhimu wa TIN Number;
Jinsi ya kufungua akaunti ya biashara;
Namna ya kutunza kumbukumbu za mapato;
Umuhimu wa kurejesha mikopo kwa wakati;
Nidhamu ya matumizi ya fedha.
Pamoja na ubunifu wa mawazo ya Biashara na namna ya kuyaandika na utekelezaji wake.
Bila elimu hiyo, hata fursa nzuri za mikopo zinaweza kubaki kuwa hadithi kwa vijana wengi kwa sababu hawataweza kukidhi vigezo vya msingi vya kuaminika na kukopesheka.
Uaminifu ni mtaji mkubwa kwa vijana
Katika dunia ya sasa, taasisi nyingi za fedha huangalia zaidi tabia ya mkopaji kuliko hata maneno yake. Vijana wakijenga utamaduni wa uaminifu, kurejesha mikopo kwa wakati na kutumia fedha kwa malengo yaliyokusudiwa, taasisi nyingi zaidi zitakuwa tayari kufungua milango kwao.
Lakini kama tabia ya kutorejesha mikopo itaendelea, hata mipango mizuri ya uwezeshaji inaweza kupoteza ufanisi kutokana na kukosekana kwa imani kutoka kwa wakopeshaji.
Kwa ujumla, mpango wa mikopo kupitia Mfuko wa Utamaduni ni fursa muhimu kwa maendeleo ya vijana nchini.
Kilichobaki sasa ni kuongeza elimu, kupunguza vikwazo visivyo lazima na kujenga uwajibikaji kwa vijana ili fursa hiyo iweze kuleta matokeo chanya kwa taifa na kizazi cha sasa cha vijana.
Maoni na Ushauri- 0713410676/ 0627869841
