Na Mwandishi wetu, Simanjiro
WANAFUNZI wanamichezo 60 wa shule za msingi wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro wamechaguliwa kuiwakilisha Wilaya hiyo kwenye Umoja wa Michezo na Taaluma Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) katika ngazi ya Mkoa wa Manyara.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Gracian Max Makota akizungumza wakati akizindua rasmi michuano hiyo katika viwanja vya Mnyalu Complex Mji mdogo wa Mirerani amewaasa wanamichezo hao wanawawakilishe vyema na kuwa washindi katika ngazi ya Mkoa.
“Mrudi na vikombe vya ushindi, mkashindane kwa akili, nguvu maarifa na nidhamu, kwani mchezaji mzuri ni yule ambaye anawasikiliza walimu na kutekeleza yale anavyoelezwa ili kufanikisha ushindi,” amesema DED Makota.
Afisa Elimu Msingi na Awali wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Darous Daudi Limandola amesema wanamichezo 60 wataiwakilisha Halmashauri hiyo kwenye ngazi ya Mkoa wa Manyara.
Limandola amesema wanamichezo hao ni timu iliyosheheni hivyo wanatarajia watarudi na ushindi katika michezo mbalimbali watakavyopambana na wanafunzi wengine wa halmashauri nyingine za mkoa huo.
“Hii ni timu ya ushindi Simanjiro ambayo tunatarajia baadhi ya wachezaji watateuliwa na kushiriki katika timu ya Mkoa wa Manyara kwenda kwenye mashindano ya UMITASHUMTA ngazi ya Taifa,” amesema Limandola.
Mratibu wa kambi ya michezo ya UMITASHUMTA ngazi ya Wilaya ya Simanjiro, mwalimu Mshana ametaja michezo itakayopambaniwa na wanafunzi 60 watakaoiwakilisha Simanjiro ngazi ya Mkoa wa Manyara ni soka la wavulana na wasichana, mpira wa pete, mpira wa wavu, riadha, miruko na mitupo, kurusha kisahani na fani za ndani.
Mwalimu Mshana amesema wamekaa kambini kwa siku 10 na wanafunzi hao wanamichezo wakiendelea kufanya mazoezi na kufundishwa na makocha wao.

