NA DENIS MLOWE IRINGA
DIWANI wa Kata ya Ilole, Erick Kikoti ameongoza mkutano mkubwa wa hadhara katika Kijiji cha Lundamatwe kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi na kutoa taarifa za utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali ya kata hiyo.
Mkutano huo ulihudhuriwa na mamia ya wananchi kutoka vitongoji vya Lundamatwe pamoja na maeneo mengine ya kijiji, ambao walifika kupata majibu ya changamoto zao na kusikia taarifa mpya za maendeleo.
Wananchi walipata nafasi ya kueleza kero zao mbele ya diwani, wakieleza changamoto za huduma muhimu kama maji, umeme, barabara, afya pamoja na masuala ya ardhi ambayo yamekuwa yakiibua migogoro mara kwa mara.
Diwani Kikoti aliwapongeza wananchi kwa kujitokeza kwa wingi katika mkutano huo, akisema ushiriki wao unaonyesha namna wanavyothamini maendeleo ya maeneo yao na uwajibikaji kwa serikali yao.
Akizungumza katika mkutano huo, Diwani Kikoti alisema dhamana waliyoimpa mwaka jana ndiyo inayomfanya kusimama imara kuhakikisha sauti za wananchi zinasikika katika kila ngazi ya maamuzi.
Alifafanua kuwa nafasi ya udiwani ni ya kuwatumikia wananchi na siyo kuwatawala, hivyo ataendelea kuwa karibu na wananchi katika kukusanya maoni, malalamiko na mapendekezo yao.
Diwani huyo alieleza kuwa ushiriki mzuri wa wananchi katika uchaguzi wa Oktoba 29 mwaka jana, ambapo walimchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, Mbunge wa eneo hilo Lita Kabati pamoja na yeye kama diwani, ni uthibitisho wa imani waliyonayo kwa viongozi wao na mwendelezo wa utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi katika ngazi ya kata.
Katika upande wa maendeleo, diwani alitoa taarifa za miradi mbalimbali inayotekelezwa au iliyo katika hatua za maandalizi katika Kijiji cha Lundamatwe na maeneo ya jirani. Alieleza kuwa mradi wa umeme katika Kitongoji cha Mjimwema umekamilishiwa ukaguzi na wataalamu, na utekelezaji unatarajiwa kuanza muda si mrefu, jambo ambalo litasaidia wakazi kupata huduma hiyo muhimu kwa shughuli zao za kiuchumi na kijamii.
Aidha, Diwani Kikoti alisema mradi wa maji katika Kijiji cha Kibati wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 200 uko katika hatua za mwisho za maandalizi kabla ya kuanza kutekelezwa.
Alifafanua kuwa kukamilika kwa mradi huo kutapunguza kwa kiasi kikubwa adha ya upatikanaji wa maji safi ambayo imekuwa changamoto kubwa kwa wananchi wanaotumia muda mwingi kufuata huduma hiyo katika maeneo ya mbali.
Katika hatua nyingine, diwani alizungumzia mradi mkubwa unaotarajiwa kutekelezwa katika eneo la Mashamba ya Mkoa yaliyoko Viwengi ambao unahusisha ujenzi wa maegesho ya zaidi ya malori 80, kituo cha mafuta, maduka na hoteli.
Alisema mradi huo, wenye thamani ya shilingi bilioni 5.9, tayari umepangiwa shilingi milioni 700 kwa awamu ya kwanza na ujenzi unatarajiwa kuanza mwezi wa sita mwaka huu. Aliongeza kuwa zaidi ya shilingi bilioni 5 zinatolewa na Serikali, huku Halmashauri ikichangia shilingi milioni 900 katika utekelezaji wa mradi huo.
Diwani Kikoti aliwataka wananchi kuwa walinzi wa miradi hiyo na kutoruhusu watu wasiokuwa na nia njema kuivamia au kujaribu kuhujumu maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo.
Alisisitiza kuwa miradi hiyo inalenga kuongeza ajira, kukuza uchumi wa maeneo ya Lundamatwe na kata nzima ya Ilole, hivyo ni muhimu wananchi washiriki kuilinda na kutoa taarifa kwa viongozi pale wanapoona dalili za uvunjifu wa taratibu.
Aidha, aliwataka wananchi kuendelea kushirikiana na viongozi wa vitongoji, kijiji na kata katika kusimamia utekelezaji wa miradi ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.
Alisema usimamizi wa pamoja baina ya viongozi na wananchi ndiyo njia pekee ya kupata maendeleo endelevu na yenye tija.
Diwani Kikoti alieleza kuwa milango yake iko wazi kwa wananchi wote wanaohitaji kuwasilisha malalamiko, maoni au mapendekezo kuhusu maendeleo ya maeneo yao.
Aliahidi kuendelea kufanya mikutano ya hadhara mara kwa mara ili kuhakikisha mawasiliano kati ya serikali na wananchi yanabaki kuwa ya wazi na yenye kujenga.

