*Wadau wa Sekta ya Madini Waendelea Kununua Crucibles za GST
Dodoma – Mbwanga
Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imeendelea kushuhudia ongezeko kubwa la mahitaji na ununuzi wa vyungu maalumu vya uchunguzi wa sampuli za madini ya metali (crucibles) vinavyozalishwa na taasisi hiyo, hatua inayolenga kuimarisha shughuli za uchunguzi wa madini nchini na kuongeza ufanisi katika sekta ya madini.
Akizungumza wakati wa zoezi la upakiaji wa vyungu hivyo tayari kwa kusafirishwa kwenda kwa wateja mbalimbali, Mkurugenzi wa Huduma za Maabara wa GST, Bw. Notka Banteze, amesema mradi huo ni sehemu ya jitihada za taasisi katika kutoa suluhisho la ndani kwa maabara za uchunguzi wa madini nchini, jambo linalorahisisha shughuli za uchunguzi wa madini kwa wachimbaji wadogo, wa kati pamoja na migodi mikubwa.
Bw. Banteze amesema vyungu hivyo vinazalishwa kwa kutumia malighafi zinazopatikana hapa nchini pamoja na utaalamu wa wataalamu wa ndani wa GST, hatua inayochochea matumizi ya teknolojia ya ndani na kuongeza thamani ya rasilimali za Tanzania.
“Tunawakaribisha wadau wote wa sekta ya madini kutumia vyungu hivi ambavyo vina ubora wa hali ya juu. Mradi huu umebuniwa na wataalamu wetu wa ndani, tunatumia malighafi za hapa nchini, na vyungu hivi vina uwezo wa kuhimili joto hadi nyuzi joto za sentigredi 1,400,” amesema Bw. Banteze.
Amefafanua kuwa vyungu hivyo vinazalishwa katika ukubwa (sizes) nne tofauti ambazo ni D30, D40, D50 na D55, ili kukidhi mahitaji mbalimbali ya uchunguzi wa sampuli za madini katika maabara na migodi.
Kwa mujibu wa Bw. Banteze, mzigo wa vyungu vyenye ujazo wa D55 una zaidi ya vyungu 7,000 vyenye uzito wa takribani tani sita, ulikuwa tayari kwa ajili ya kusafirishwa kwenda kwa wateja wa Kanda ya Ziwa baada ya kukamilisha malipo yao.
Aidha, amesema moja ya faida kubwa ya vyungu hivyo ni uwezo wake wa kutumika zaidi ya mara tatu katika shughuli za uchunguzi wa sampuli za madini, hali inayosaidia kupunguza gharama kwa watumiaji huku ikiongeza ufanisi na ubora wa matokeo ya uchunguzi wa maabara.
Katika hatua nyingine, Bw. Banteze ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuiwezesha GST kwa vifaa vya kisasa vya uzalishaji. Amesema kwa sasa taasisi inamiliki mashine yenye uwezo wa kuzalisha hadi vyungu 800 kwa siku, hatua inayoongeza uwezo wa uzalishaji na kusaidia kukidhi mahitaji makubwa ya soko.
Mbali na uzalishaji wa vyungu hivyo, Maabara ya GST yenye ithibati imeendelea kutoa huduma mbalimbali za uchunguzi na upimaji wa sampuli za miamba na madini kwa kutumia teknolojia za kisasa. Huduma hizo ni pamoja na uchunguzi wa malighafi zinazotumika katika sekta ya ujenzi kupitia taaluma ya Geo-technical Engineering, pamoja na uchunguzi wa sampuli kwa ajili ya tafiti za uchenjuaji wa madini (Metallurgical Tests).
Pia ametoa wito kwa wadau wote wenye maabara za uchunguzi wa sampuli za madini nchini kutumia bidhaa hiyo mpya ya ndani, akisisitiza kuwa bei yake ni nafuu, ubora wake umehakikishwa, na huduma ya usafirishaji inapatikana kwa urahisi katika maeneo mbalimbali nchini.

