NA: MWANDISHI WETU, PANGANI

Walimu na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Funguni ya wilayani Pangani mkoani Tanga wamenufaika na elimu kuhusiana na ugonjwa wa Ebola.

Elimu hiyo imetolewa Mei 22, 2026, na Jackline Mjema ambaye ni Afisa Afya kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa wilaya hiyo alipozungumza na walimu na wanafunzi hao.

Katika maelezo yake, Mjema ameeleza kuwa ugonjwa huo huambukizwa na virusi vya Ebola ambapo chimbuko lake lilianzia kwa wanyama wa porini aina ya sokwe na nyani nchini Kongo. 

Vilevile, alieleza dalili za ugonjwa huo kuwa ni homa kali, macho kuwa mekundu, maumivu ya kichwa, koo na misuli, kutoka damu puani, masikioni au mdomoni.

“Ni vyema mkanawa mikono yenu kwa sabuni na maji tiririka muwapo shuleni na nyumbani, kuepuka kushika matapishi, mate au majimaji kutoka kwa mgonjwa,” alisisitiza Mjema.

Vilevile, alishauri kuepuka kula nyama mbichi au ambazo hazijaiva vizuri, huku akisisitiza chakula kipikwe na kuiva vizuri ndipo kiliwe. 

Njia nyingine za kujikinga ni kuepuka mahusiano ya kimapenzi na kushiriki mazishi bila uwepo wa wataalamu wa afya.

Sanjari na hilo, Mjema alisisitiza shule hiyo kuweka ndoo na sabuni ili wanafunzi waweze kunawa mikono yao mara kwa mara ili kuwa salama zaidi.

Akitoa neno la shukrani, Makamu Mkuu wa Shule, Masoud Abdallah alishukuru elimu iliyotolewa kwani imewasaidia walimu na wanafunzi kuwa na uelewa mpana wa ugonjwa wa Ebola. Pia, alishauri walimu na wanafunzi na hao kusambaza elimu waliyoipata kwa wengine.

Kimsingi, Ebola ni ugonjwa hatari wa kuambukiza ambao hauna dawa na huua wagonjwa wengi, huku ushauri wa kwenda mapema katika vituo vya afya ukisisitizwa pindi dalili za ugonjwa huo zikionekana kwa mtu.

Halmashauri ya wilaya ya Pangani imejizatiti kuyafikia makundi mbalimbali mashuleni, masokoni, vituo vya mabasi ili kuwajengea uelewa wananchi kujikinga na ugonjwa huo hatari.