Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude akizungumza kwenye uzinduzi huo jijini Arusha
Mkurugenzi wa  Kampuni ya Loti Energies Bw. Collins Kimaro  akizungumza kwenye uzinduzi huo jijini Arusha 
………….
Na Happy  Lazaro, Arusha 
Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude,amezindua rasmi chapa yake  mpya ya gesi safi ya kupikia, LOTI GAS,huku akisisitiza umuhimu wa matumizi ya nishati safi kwa maendeleo ya afya, mazingira na uchumi wa wananchi.
Aidha Mkuu wa wilaya  huyo ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. CPA Amos Makalla amewataka wananchi hao kutumia nishati hiyo kwa wingi ili kutunza mazingira.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkude ameipongeza kampuni ya LOTI GAS kwa uwekezaji wake ambao amesema unaenda sambamba na dira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa lengo la kupunguza matumizi ya kuni na mkaa ili kulinda mazingira pamoja na afya za wananchi.
Mkude amesema mwitikio wa matumizi ya nishati safi nchini umefikia asilimia 28.6, huku juhudi mbalimbali zikiendelea kuhakikisha taifa linafikia malengo yaliyojiwekea katika sekta hiyo muhimu.
“Uwekezaji wa kampuni ya LOTI GAS umefungua fursa za ajira kwa vijana na kuchangia kukuza uchumi wa Mkoa wa Arusha pamoja na taifa kwa ujumla.”amesema Mkude .
Aidha ameihimiza menejimenti na watumishi wote wa LOTI GAS kuhakikisha wanazingatia viwango vya usalama, ubora wa bidhaa pamoja na kutoa huduma bora kwa wateja ili kujenga imani kwa wananchi.
“Nawasihi wananchi wa Arusha na Watanzania kwa ujumla kuchangamkia fursa ya matumizi ya nishati safi, akibainisha kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji wenye nia njema ili kuweka mazingira bora ya biashara na maendeleo nchini.”amesema Mkude .
Akizungumza kwenye uzinduzi huo ,Mkurugenzi wa Loti Energies Bw. Collins Kimaro amesema kuwa , dira ya kampuni hiyo ni  kuona Tanzania ambayo kila nyumba—kuanzia  Arusha hadi maeneo ya vijijini—inaweza kutumia nishati safi ya kupikia kwa usalama, kwa upatikanaji rahisi na kwa gharama  rafiki.
Aidha amefafanua kuwa ,  tofauti ya Loti Gas ni kwamba inakuletea amani kwani  afya inalindwa kwa sababu hamna moshi,mitungi misafi na mipya na amani kutokana na usalama, imepimwa na ina vigezo vyote na ni bei rafiki.
Aidha ameongeza kuwa,gas hiyo inapatikana kwa urahisi, madukani au kwa delivery .ambapo mteja anapelekewa sehemu yoyote.
“Uzinduzi huu umefanyika chini ya kampeni ya “Tupo Jikoni na Loti – Gesi ya  Kuaminika Kwako”, ambapo uzinduzi huo  umeambatana na shindano la kupika supu lililoonyesha  matokeo mazuri na ladha ya kuvutia, kuthibitisha ubora wa Loti Gas katika matumizi ya kila siku.”amesema  Mkurugenzi Kimaro.
Uzinduzi huo ambao umefanyika katika ukumbi wa  Aim Mall Arusha ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali ambao kwa pamoja  wamepongeza kampuni ya Loti Energies kwa uwekezaji huu inayounga mkono malengo ya serikali ya kuendeleza nishati safi ya kupikia kwa Watanzania wote.
“Uzinduzi ulionyesha pia uwepo wa wakala wengi wa Loti Gas, jambo linalothibitisha  kuwa tayari Loti Gas imeanza kupatikana sokoni Arusha, ikiwa na mitungi ya kilo 6 na 
kilo 15, na mpango wa kupanua zaidi kadri mahitaji yanavyoongezeka.” amesema Kimaro.